TAHARIRI: Kura si mwisho wa maisha, tulinde utu

KITENGO CHA UHARIRI

UCHAGUZI mdogo katika eneobunge la Kiambaa na Wadi ya Muguga katika Kaunti ya Kiambu umekuwa gumzo kubwa la kisiasa na uliteka mawazo na hisia za wengi kwa miezi michache iliyopita.

Kura hiyo ilionekana kama vita vya kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na rafiki yake wa zamani wa kisiasa Naibu Rais William Ruto.

Makabiliano hayo kati ya vigogo hawa wa kisiasa yamefanyika ikiwa imesalia miezi 13 tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao. Kampeni za mwaniaji wa ubunge Kiambaa kwa tiketi ya Jubilee Bw Kariri Njama zilifanywa kwa juhudi kubwa, ikiwemo msaada mkubwa kutoka kwa chama chake cha Jubilee huku juhudi za juu zaidi zikifanywa na wafuasi wa Ruto kwa mpeperushaji wa bendera ya UDA Bw John Wanjiku.

Kwa kweli, kambi zote zilidai kuwa matokeo yangeonyesha jogoo wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.

Kwa miezi michache sasa, wakazi wa Kiambaa na Muguga walishuhudia kampeni zenye umahiri mkubwa za wawaniaji wao tofauti. Kampeni hizo zilikuwa za amani huku kambi pinzani zikikutana barabarani, bila picha mbaya kuripotiwa.

Baada ya uchaguzi wa juzi, mgombea wa UDA wa Ruto alishinda Kiambaa, wakati mtu wa Uhuru wa Jubilee alipata kiti cha Wadi ya Muguga. Tofauti ya kura ilikuwa 510 Kiambaa na 27 katika Wadi ya Muguga. Demokrasia ilishinda, na sauti ya watu imesikika debeni.

Hata hivyo, mwenendo hatari ulishuhudiwa katika mitandao ya kijamii, ambapo viongozi kadhaa walichapisha madai mengi ambayo hayajathibitishwa. Kutoa madai ya kutisha na picha, inaweza kuchochea wapiga kura dhidi ya kila mmoja au dhidi ya maafisa wa uchaguzi.

Viongozi kadhaa na watu mashuhuri walichapisha madai ya udanganyifu uliopangwa, hongo na vitisho vya wapiga kura kabla ya uchaguzi mdogo. IEBC na taasisi za kisheria hazipaswi kupuuza, haswa tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao.

Wahalifu wa uchaguzi wanapaswa kuitwa na kuadhibiwa vikali kabla ya kipindi cha uchaguzi ujao. Uchochezi na madai yasiyothibitishwa yanaweza kusababisha vurugu za kabla au baada ya uchaguzi. Na kwa kuja kwa majukwaa ya mitandao ya kijamii, ni rahisi kwa watu wazembe kuchochea umati.

Habari zinazohusiana na hii