TAHARIRI: Kususia kura si jibu la kupata uongozi bora

TAHARIRI: Kususia kura si jibu la kupata uongozi bora

NA MHARIRI

KENYA hivi leo, kwa mara nyingine, itafanya shughuli muhimu itakayoamua hali itakavyokuwa katika siku na miaka ya usoni.

Sawa na jinsi ilivyo kila baada ya miaka mitano, Wakenya waliosajiliwa kupiga kura watashiriki katika Uchaguzi Mkuu.

Taifa hili limepiga hatua kubwa katika masuala ya kidemokrasia tangu lilipopata uhuru kutoka kwa wakoloni.

Licha ya changamoto za hapa na pale kuhusu uongozi bora, wananchi wote waliojisajili kupiga kura hawafai kufa moyo bali wajitokeze kujiamulia viongozi wanaowataka.

Kura za maoni zilizofanywa na mashirika mbalimbali zinatia wasiwasi kuhusu idadi ya watu ambao, kufikia wiki iliyopita, walikuwa bado hawajaamua iwapo watashiriki katika uchaguzi, hasa wa rais.

Katika mahojiano ambayo baadhi ya wananchi hufanyiwa na vyombo vya habari, utakuta sababu zinazotajwa na wale ambao wanataka kususia kura ni kama vile kutokuwa na matumaini kwa viongozi wa kisiasa kuboresha maisha ya umma, ufisadi katika sekta zinazotegemewa kutoa huduma kwa wananchi, matumizi ya pesa za umma kwa masuala yasiyo na msingi, miongoni mwa mengine.

Ni wazi kuwa wananchi wana kiu ya uongozi bora ambao utawaboreshea maisha yao na vizazi vyao vijavyo.

Kususia kura hutajwa na wataalamu wa kisiasa na wanaharakati kuwa njia mojawapo ya raia kupinga ukosefu wa uongozi bora.

Hata hivyo, njia ya busara ya mwananchi kuonyesha amechoshwa na uongozi mbaya sio kususia kura, bali kujitokeza na kumchagua kiongozi yule ambaye amedhihirisha ana uwezo wa kutumikia wananchi bila ubinafsi.

Hili limewahi kuthibitika katika mataifa ya nje ambapo wananchi walijitokeza na kuchagua viongozi ambao kamwe hawangetarajiwa kushinda.

Mbali na wananchi, wito wetu unaelekezwa pia kwa wadau wakuu wanaohusika katika maandalizi ya uchaguzi huu.

Kenya husifiwa kimataifa kwa kuwa mstari wa mbele kujiendeleza katika sekta mbalimbali za utoaji huduma kisasa, hasa kupitia mitandao ya kiteknolojia.

Barani Afrika, nchi hii ni mojawapo ya machache ambayo yamekumbatia teknolojia kuandaa na kusimamia uchaguzi wa viongozi wa kisiasa. Katika miaka iliyopita, tume ya IEBC ilikumbwa na changamoto mbalimbali wakati matumizi ya teknolojia yalipoanzishwa uchaguzini.

Ni matumaini yetu kwamba, katika maandalizi ya uchaguzi wa leo Jumanne, changamoto ambazo ziliibuka miaka iliyopita zilitumiwa kama funzo ili ziepukike safari hii.

Vilevile, tunatoa wito pia kwa idara ya usalama kuhakikisha matukio ya kutisha yaliyoshuhudiwa miaka iliyopita, hayatarudiwa.

Polisi watekeleze majukumu yao ya kutoa ulinzi kwa njia za kiutu ambazo hazitaweka hatarini maisha ya wananchi wasio na hatia yoyote.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Vijana wapuuze wanasiasa wakiwachochea...

Kafyu yasitishwa Marsabit, Kerio kuwezesha kura

T L