Makala

TAHARIRI: Lazima ukatili wa walimu ukabiliwe

May 28th, 2018 2 min read

Na MHARIRI

POLISI wanapaswa kuharakisha na kuwatia mbaroni walimu wawili wa shule moja ya msingi katika kaunti ya Nyandarua, wanaosemekana kushirikiana na mwenzao wa tatu kumjeruhi mtoto mdogo katika sehemu zake nyeti.

Inasemekana kuwa watatu hao katika shule ya msingi cha Kamukunji, walitoroka baada ya kumjeruhi mtoto huyo, huku ikidaiwa kuwa mmoja wao alimpiga teke katika sehemu zake za kiume.

Madaktari katika hospitali ya rufaa ya Nyahururu walithibitisha kuwa mtoto huyo aliraruliwa sentimita sita katika korodani.

Kisa hiki ni kimoja kati ya vingi vya unyama vinavyoendelezwa na walimu katika shule za umma nchini. Ni unyama na jambo la kuudhi kwamba watu waliopewa jukumu la kuwaelimisha na kuwalinda watoto katika shule zetu za umma wanageuka na kuwa makatili.

Mamilioni ya Wakenya ni watu wa mapato ya kawaida na hutegemea huduma zinazopatikana katika taasisi za umma. Kwa hivyo hawana sehemu nyingine ya kupeleka watoto wao kusoma isipokuwa katika shule za umma.

Isitoshe, ni haki ya kila Mkenya kusomeshewa mwanawe na serikali, kwa kuwa shule hizo za umma zinafadhiliwa kupitia ushuru anaotozwa.

Ili kuhakikisha kuwa shule hizo zinakuwa salama, Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) inapaswa kuchukua hatua za haraka na kuchunguza mienendo ya watu wanaotaka kuwa walimu.

Badala ya pendekezo lake kwamba walimu wapya waandike mkataba wa kuhudumu kwa angalau miaka mitano, TSC yafaa kuchunguza mienendo ya walimu wapya.

Waliosema ukicha mwana kulia mwisho utalia wewe, hawakuwa na maana kwamba mtoto mdogo wa miaka saba anastahili kuchapwa viboko katika sehemu nyeti.

Huu sio tu ukiukaji wa maadili ya utendakazi wa walimu, bali pia ni uvunjaji wa sheria kuhusu haki za watoto.

Kitengo cha nidhamu cha TSC chapaswa kuwachukulia hatua walimu watatu waliohusika katika kisa cha Nyandarua na wengine wengi wenye tabia sawa na hizo.

Hatukatai kwamba mtoto anastahili kurekebishwa tabia, lakini si kwa njia ya ukatili kama ya washukiwa.

Katika karne hii ambapo wananchi wameerevuka, itakuwa vyema kwa polisi na idara ya mahakama kuharakisha kuadhibiwa kwa washukiwa.

Hasira zilizowapanda wananchi ni za kiwango cha juu, na haitakuwa salama wa washukiwa kuendelea kuwa huru mitaani.

 

Ni tovuti ya Gazeti la Kampuni ya Nation Media Group
Mkurugenzi Mkuu: STEPHEN GITAGAMA
Mhariri Mkuu: TOM MSHINDI
Mhariri : PETER NGARE