Makala

TAHARIRI: Maamuzi ya korti yaheshimiwe

January 8th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

HATUA ya Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji kutangaza kuwa wakili na mwanaharakati Miguna Miguna yuko huru kurejea nchini baada ya miezi kadha uhamishoni ni nzuri na inadhihirisha kwamba Kenya bado imo chini ya mfumo wa utawala wa sheria.

Vuta nikuvute ambayo imekuwepo kwa muda mrefu sasa kati ya asasi mbili kuu za serikali – polisi na idara ya uhamiaji kwa upande mmoja – na wakili huyo mbishani kwa upande mwingine, haikustahili kwa kuwa ilisawiri nchi hii kama taifa ambalo haliheshimu sheria.

Mahakama za ngazi tofauti zilitoa maamuzi ambayo yalimtambua Bw Miguna kama raia halisi na mzaliwa kamili wa nchi hii. Na mara kadha, maafisa serikalini walionekana kukaidi maagizo ya mahakama kumruhusu arejee nyumbani kutoka uhamishoni Canada ambapo familia yake inaishi.

Hali ilibadilika ghafla baada ya Rais Uhuru Kenyatta, kwa kejeli kurejelea safari ya mwanaharakati huyo ya kurejea nyumbani Jumanne akisema wote wanaofoka ugenini wako huru kurejea nyumbani na kuendelea ‘kupiga domo’.

Kwa kweli wakati umefika kwa taifa hili kuheshimu sheria na taasisi zake badala ya kutegemea hisia na maamuzi ya kiongozi binafsi.

Rais Kenyatta ndiye kiongozi wa nchi na usemi wake katika maswala ya kitaifa ni muhimu. Lakini uamuzi wake haufai kuwa na uzito zaidi ya uamuzi wa mahakama.

Katika nchi zinazokumbatia mfumo wa utawala wa demokrasia, mahakama ndio mwamuzi wa mwisho kwenye mizozo. Yamkini, hali ni tofauti nchini ambapo idara zote husubiri maoni ya kiongozi wa taifa kabla ya kuchukua hatua.

Kwa muda mrefu sasa, mahakama zetu zimekuwa zikitoa maagizo ambayo maafisa wakuu wa serikali wanakaidi. Kwa mfano, ni wazi kwamba, idara nyingi za seikali hazilipi ridhaa kwa wale wanaowasilisha kesi kortini na kushinda baada ya kudhulumiwa au haki zao za kimsingi kukiukwa.

Hali kama hii hushuhudiwa katika mataifa yanayoongozwa na madikteta au mfumo wa sheria hauna nguvu zozote.

Tunachosema hapa ni kwamba, Kenya ni nchi yenye katiba, inayoongozwa na sheria na hivyo maamuzi yoyote ya korti yanapasa kuheshimiwa bila kutegemea hisia za viongozi wetu.