Makala

TAHARIRI: Mabadiliko makubwa yafanywe katika KFS

October 30th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

RIPOTI kuhusu uozo unaosakama shirika la huduma za feri nchini (KFS) ni za kuhuzunisha na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kurekebisha hali hiyo.

Mbali na taarifa kwamba feri iliyosababisha kuzama kwa gari na kufariki kwa mwanamke na bintiye wiki chache zilizopita iligunduliwa kuwa na shimo lililokuwa likiingiza maji na hivyo kuhatarisha maisha ya maelfu ya abiria wanaoitumia kila siku, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Bw Abdalla Gowa alifichua habari za kukeketa maini Jumanne.

Alisema feri zote zinazomilikiwa na shirika hilo kwa sasa hazifai kwa matumizi kwa mujibu wa kanuni za shirika la kusimamia vyombo na usalama baharini.

Bw Gowa anadai shirika hilo halina raslimali za kutosha kununua feri mpya. Hivyo wakuu hao wanalazimika kutumia feri ambazo zimepigwa marufuku kwingineko kusafirisha maelfu ya raia kila siku.

Kwa kweli huu ni utepetevu mkubwa kazini na uhalifu wa hali ya juu. Hakuna sababu yoyote itawafanya wasimamizi wa shirika muhimu kama hilo kuweka maisha ya raia kwenye hatari kila siku, kama anavyofanya Bw Gowa na wasimamizi wenzake katika KFS.

Kwa mujibu wa mashirika yanayosimamia vyombo vya majini, feri inapaswa kusitisha huduma zake baada ya kuhudumu kwa saa 30,000 majini. Kwa vigezo hivyo, feri zote sita ambazo zinahudumu kwenye vifuko vya Likoni, Mombasa hazipaswi kuruhusiwa kuhudumu.

Isitoshe, feri za sasa zimo katika hali mbaya ya kiufundi. Kama Wakenya walivyoshuhudia wiki chache zilizopita wakati Bi Kighenda na mwanawe Amanda walitumbukia baharini, kuna uwezekano wa janga baya hata zaidi kutokea iwapo uzembe uliopo miongoni mwa wakuu wa shirika hilo utaruhusiwa kuendelea.

Katika mataifa yaliyostaarabika, Bw Gowa na wenzake wangekuwa wamejiuzulu na kuomba Wakenya msamaha kwa kukubali majukumu ambayo hawana ari wala uwezo wa kuyatekeleza.

Kwa misingi hiyo, Wizara ya Uchukuzi ambayo pia ni mhusika mkuu katika uozo huo inapasa kuchukua hatua za haraka kuwatimua wasimamizi wa shirika hilo.

Halitakuwa jambo la busara kusubiri hadi mkasa mwingine utokee ndipo serikali ichukue hatua. Maisha ya Wakenya ni muhimu kuachwa mikononi mwa maafisa wazembe, walafi na wasiojali nafsi za wanadamu wenzao. Huu ndio wakati mwafaka kwa Waziri James Macharia kufagia kombamwiko waliotapakaa kwenye shirika la Kenya Feri Services.