Makala

TAHARIRI: Magavana wanacheza na maisha ya Wakenya

July 29th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

MAAMBUKIZI ya virusi vya corona yanaendelea kuongezeka na kutishia kulemaza taasisi za matibabu nchini.

Katika takwimu za hivi punde zaidi, watu takribani 950 waliambukizwa virusi hivyo ambavyo kufikia sasa havina kinga wala tiba.

Serikali kuu imejikakamua kuhakikisha maambukizi yanadhibitiwa na wale walioambukizwa wanapokea matibabu kwa wakati unaofaa.

Hivyo basi, ni jambo la kusikitisha kwamba baadhi ya magavana nchini wameamua kulichukulia suala la maambukizi kimzaha.

Baadhi wameamua kutoa taarifa za kupotosha kuhusu maandalizi yao kukabiliana na ueneaji wa virusi hivyo ambavyo vimetetemesha mataifa mengi, hasa ya Magharibi.

Wakati Rais Uhuru Kenyatta aliwahimiza magavana kujiandaa kuhudumia waathiriwa zaidi baada yake kufungua mipaka ya kaunti zilizoathiriwa zaidi na maambukizi, baadhi ya magavana waliamua kutumia mbinu chafu kuhakikishia Rais na nchi kwa jumla kwamba, wako tayari kabisa kushughulikia wale watakaoambukizwa virusi hivyo.

Kimsingi, waliamua kudanganya kuhusu uwezo wao wa kuhudumia wagonjwa wa Covid-19.

Katika hali ya kushangaza, baadhi ya magavana waliokota vitanda kutoka shule za mabweni na kudai kwamba wako tayari kupokea wagonjwa wa Covid-19.

Wengine walaghai walikodisha vitanda kutoka kwa taasisi za afya za kibinafsi kwa lengo la kufurahisha maafisa wa kitengo maalumu kilichokuwa kinakagua maandalizi ya kaunti kuhudumia wagonjwa hao.

Isitoshe, baadhi ya magavana waliwasilisha stakabadhi za kuonyesha wameagiza vitanda na mitambo maalumu ya kuhudumia wagonjwa mahututi bila vifaa hivyo kuwasilishwa.

Kwingineko, kamati hiyo iligundua kwamba, mfumo mzima wa afya katika baadhi ya kaunti ulikuwa umesambaratika.

Hali ya kucheza karata na maisha ya Wakenya haifai, na magavana husika wanapasa kuaibishwa hadharani ili wawajibike zaidi.

Tunapongeza magavana wa kaunti za Kakamega, Mombasa, Machakos, Murang’a na Kiambu ambao walichukulia kwa uzito wito wa Rais na kujiandaa kikamilifu kukabiliana na janga hili.

Kuna mengi ya kujifunza kutokana na idadi kubwa ya raia wa mataifa kama Amerika, Brazil na hata Afrika Kusini wanaopoteza maisha yao kutokana na ugonjwa huu. Maandalizi ya mapema ni kama kinga na kinga ni bora kuliko tiba.