Makala

TAHARIRI: Malumbano haya yasiue ndoto ya BBI

December 1st, 2019 2 min read

NA MHARIRI

Ilipozinduliwa mnamo Jumatano wiki hii, ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) ilionekana kutoa mwelekeo ambao Wakenya wanahitaji katika kuunganisha nchi yao.

Wito ulitolewa na wote waliohudhuria wakiwemo kutoka nchi jirani kuwa pawepo mdahalo wa kitaifa ili kuifanikisha ripoti hiyo.

Lakini kauli zilizofuatia zinaonyesha kuwa ikiwa wanasiasa hawatabadilisha misimamo nchi haitatimiza malengo yake.

Kuna hatari kwamba itaacha Wakenya wakiwa wamegawanyika zaidi na hii ni hatari kwa nchi hii. Ingawa kila mmoja ana haki ya kutoa maoni yake, matamshi ya wanasiasa yanawavunja moyo raia ambao walitarajia kuona ikabadilisha nchi kupitia mchakato uliokubaliwa na pande zote.

Inaonyesha wazi himizo la wanasiasa kutoteka ripoti hiyo liliishia katika ukumbi wa Bomas of Kenya wajumbe zaidi ya 4000 walipokusanyika.

Ikiwa kweli nia ya wanasiasa ni kuona nchi bora yenye uwiano, utangamano na ushirikishi wanafaa kuepuka misimamo inayoweza kuyeyusha lengo la ripoti hii.

Ikiwa Wakenya wanataka kuchukua usukani wa mchakato huu, wanafaa kuwapuuza wanasiasa, wasome ripoti hiyo na kuamua mwelekeo wanaotaka kuona nchi ikichukua.

Imetendeka katika nchi tofauti na raia wamefaulu kwa kuonyesha kuwa mamlaka ni yao na sio ya wanasiasa.

Itakuwa vyema pia iwapo waasisi wa mchakato huu, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wangechukua usukani na kuwaelekeza wanachama wa kambi zao ili kuepuka mtafaruku wa kimaoni.

Viongozi hao wawili wamekuwa wakieleza Wakenya kwamba wanampango mkubwa na mzuri wa kuunganisha nchi na kwa hivyo iwapo ripoti hii itaenda kinyume na hakikisho lao watakuwa wa kulaumiwa.

Inashangaza kuona uvumilivu ukikosekana kwenye mikutano hadi wanasiasa wanarushiana maneno kwenye mikutano ya hadhara kwa sababu ya ripoti inayonuiwa kuunganisha nchi.

Itakuwa aibu ikiwa wanasiasa watatumiwa kulemaza juhudi za kufanya Kenya kuwa bora zaidi. Itakuwa aibu kwa mchakato ulioungwa mkono na jamii ya kimataifa ukisambaratika kwa sababu ya tamaa ya wanasiasa wachache.

Wanapolumbana, ni matumaini yetu kwamba Wakenya wanawapiga darubini wawakatae kwenye uchaguzi ujao.

Na ni matumaini yetu kwamba hali haitakuwa mbaya kiasi cha kuzuia Wakenya kupata huduma. Kila mmoja abadilishe msimamo na kufikiria Kenya badala ya vyeo na watu binafsi na kwa nia njema.