Makala

TAHARIRI: Mara hii Chui ana kucha dhidi ya Gor

March 7th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

WATANI wa jadi AFC Leopards na Gor Mahia watakabiliana Jumapili hii ikiwa ni kwa mara ya 88 tangu timu hizo zianzishwe miaka ya sitini.

Mashabiki watakaofika ugani MISC, Kasarani watatarajia burudani tosha kutokana na sababu kwamba mechi hii imekuja wakati timu zote zinajivunia fomu nzuri. Zote zimeshinda mechi nne mfululizo kati ya tano za majuzi zaidi.

Katika mechi zao mwishoni mwa juma lililopita, Gor Mahia ambao ndio mabingwa watetezi waliichapa Western Stima 3-2, huku AFC Leopards wakiondoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Chemelil Sugar, ugenini.

Gor Mahia wanashikilia nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 51, mbele ya Kakamega Homeboyz, kwa tofauti ya pointi nne, huku zikiwa zimesalia mechi 11.

Wakiwa katika nafasi ya sita jedwalini kwa mwanya wa pointi 11 dhidi ya Gor Mahia, AFC Leopards hawajakata tamaa katika kampeni ya kutwaa ubingwa wa msimu huu.

Ingwe imekuwa na kikosi kizuri tangu msimu huu uanze baada ya kusajili mastaa kadhaa akiwemo kipa Benjamin Ochan ambaye amekuwa akitoa mchango mkubwa, huku akishirikiana vyema na mabeki wa kikosi hicho.

Vijana hao wa kocha Anthony Kimani wanatarajiwa kuvuruga matumaini ya K’Ogalo baada ya kushindwa mikondo yote miwili msimu uliopita.

Leopards iliishinda Gor Mahia mara ya mwisho mnamo 2016, ugani MISC Kasarani katika mechi ambayo ilimalizika kwa 1-0, lakini mara ya kwanza timu hizo zilipokutana mnamo 1968, Leopards wakati huo ikijulikana kama Abaluhya ilishinda 2-1.

Daima ni pambano ambalo huzua hisia nyingi miongoni mwa mashabiki wa soka nchini, sawa na Yanga na Simba SC za Tanzania au Kaizer Chiefs na Orlando Pirates nchini Afrika Kusini.

Anthony Kimani ambaye mbinu zake zimeanza kuzaa matunda baada ya kuwa na vijana hao tangu Casa Mbungo aondoke mwishoni mwa mwaka uliopita, ameeleza matumaini ya vijana wake kuvuma .

Tayari Kimani amewakumbusha mashabiki kwamba lengo lake kubwa ni kuiongoza Leopards kutwaa ubingwa wa ligi kuu (KPL) ambao waliutwaa kwa mara ya mwisho mwaka 1998, timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Mtanzania, Sunday Kayuni.