Makala

TAHARIRI: Maswali mengine hayafai katika sensa

August 25th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

SHUGHULI inayoendelea ya kuwahesabu watu inahitaji kufanyiwa marekebisho ikiwa serikali inatarajia kupata takwimu sahihi na za kuaminika.

Katika siku ya kwanza pekee, kulijitokeza changamoto nyingi ambazo zinaweza kufanya majibu ya kuhesabu watu yawe ya kutiliwa shaka, au yasitimize lengo kuu la kutambua idadi kamili ya wananchi wote.

Wataalamu wa Utafiti wa takwimu wataeleza kwamba unapotaka mtu akupe majibu sahihi, yafanye maswali yako yawe machache, mafupi na ikiwezekana yawe na majibu ya Ndio au La bila kuhitajika maelezo ya ziada.

Maafisa wanaoendeleza ukusanyaji takwimu hata wamefukuzwa katika baadhi ya maeneo nchini, kutokana na kuuliza maswali mengi, baadhi yakionekana kuwa yasiyo na msingi. Kwa kuchukua mfano wa maswali yaliyowahi kuulizwa mwaka 2009, mtu alitakiwa ajulikane kama anaishi na nani? Anafanya kazi au la? Kama ameoa na ana watoto wangapi? Je, anamiliki chochote?

Maafisa hao mwaka huu wanataka nambari ya simu, nambari ya kitambulisho na hata kama ulisoma umefikia wapi katika kiwango chako cha elimu, miongoni mwa msururu mrefu wa maswali. Kujua kiwango cha elimu cha mtu hakutaisaidia Kenya kujipanga kivyovyote, kwa kuwa serikali ina takwimu za kutosha kuwa Vyuo Vikuu kila mwaka vinatoa vijana wangapi wakiwa na shahada za aina gani.

Kama kweli serikali ingekuwa inajipanga kulingana na kufuzu kwa watu kielimu, ingelikuwa imeshatafuta suluhu kwa tatizo la ukosefu wa ajira au kutokuwepo mazingira bora ya vijana kuwekeza.

Isitoshe, baadhi ya maafisa wanachukua muda mrefu kuuliza maswali kila mtu katika nyumba. Kwa mfano mtu akiwa na watoto sita au saba, maafisa hao huuliza kila mmoja maswali, mengine yakionekana kuwa ya udaku na umbea na ambayo hayana umuhimu kwa wanaohitaji takwimu.

Kwa mfano kumuuliza mtoto anayefanya mfumo wa sasa wa CBC ambaye yupo gredi ya kwanza au ya pili akusomee alfabeti, huko ni kupoteza wakati. Muhimu kwa wizara ya Fedha na Mipango ni kujua idadi ya watu na wala si watoto wangapi wako katika darasa fulani. Habari hizi si lazima zijulikane kupitia sensa. Tayari kuna mfumo wa kuwasajili wanafunzi wote kidijitali.

Maswali yasiyoongeza faida kwenye shughuli ya kuhesabu watu hayafai na hakuna umuhimu wa kuyauliza.