Makala

TAHARIRI: Mauaji ya kiholela yamalizwe nchini

December 28th, 2018 2 min read

NA MHARIRI

MNAMO Jumamosi wiki iliyopita, wakazi wa mtaa wa Kibera walikumbwa na kisa cha kuhuzunisha wakati polisi walimpiga risasi mwanafunzi wa chuo kikuu cha kimataifa cha Leeds, kwa madai kuwa alikuwa jambazi.

Japo kuna madai kuwa Bw Cariltn David Maina, 23 ambaye aliishi na eneo la Line Saba, Kibera alikuwa amesalimu amri ili polisi hao wasimduru, maafisa waliendelea kumpiga risasi hadi kufa.

Kisa hicho kimevutia shutuma kutoka kwa umma, huku visa vya vifo vya aina hiyo vimezidi. Mwanafunzi huyo alidaiwa kuwa alikuwa akitoka kutazama kandanda alipokumbana na mauti yake.

Majirani wamesisitiza kuwa alikuwa kijana muungwana na mwadilifu na kuwa alikuwa ametembea nchini kwa likizo, lakini polisi wakashikilia kuwa hatua yao ilifaa.

Vilio vya umma, hata hivyo Desemba 26 vilimsukuma Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet kuamrisha shirika la IPOA kuchunguza mauaji ya Bw Maina kwa haraka na kuripoti.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya familia ya aliyekuwa naibu Gavana wa kaunti ya Kilifi Kennedy Kamto kuomboleza kupigwa risasi hadi kufa kwa kiongozi huyo, wakati majambazi walimvamia nyumbani kwake. Ni kisa kilichoibua manunguniko kutoka kwa viongozi na wakazi.

Katika kaunti jirani ya Mombasa, visa vya utovu wa usalama vimekuwa vikishuhudiwa kila uchao, Gavana Hassan Joho akitaka mashirika yanayohusika kuhakikisha kuwa kuna usalama kaunti hiyo.

Magenge ya kijinai nayo yamekuwa yakitawala kaunti ya Kisumu ambapo yanatumia pikipiki kuwahangaisha wakazi, kiasi cha kamishna wa kaunti hiyo kutoa amri kwa polisi kuwapiga risasi na kuua wakora hao.

Visa hivi vinaashiria utovu wa usalama ambao unashuhudiwa kote nchini, na kuna haja kwa vikosi vya usalama kubadili mbinu ya kufanya kazi. Kuna uwezekano kuwa kifo cha Bw Kamto kinaweza kuhusishwa na siasa na kifo chake ni ukumbusho wa vifo vingine vya kisiasa kama vya Jacob Juma (2016) na Chris Msando (2017) ambavyo havijawahi kutatuliwa.

Kujitolea kwa mkuu wa DCI George Kinoti na Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kupigana na ufisadi ambao ni donda sugu kunafaa kuendelezwa katika vita dhidi ya uhalifu na hali hiyo itawapa Wakenya haki. Wakenya wanafaa kuhisi salama katika taifa lao.