Makala

TAHARIRI: Mfumo mpya wa elimu uboreshwe

December 17th, 2018 2 min read

NA MHARIRI 

HATUA ya Wizara ya Elimu kuahirisha kwa ghafla utekelezaji wa Mfumo Mpya wa Elimu hadi mwaka 2020 inazua maswali kuhusu mchakato mzima wa utayarishaji wa mfumo huo.

Mnamo Jumamosi, Waziri wa Elimu Amina Mohamed aliwashangaza wengi baada ya kutoa tangazo la ghafla kwamba serikali imeamua kuahirisha utekelezaji wake baada ya mashauriano ya kina na wadau wa elimu.

Hata hivyo, iliibuka kwamba mfumo huo haungefaulu, baadhi ya wadau wakidai kutoshirikishwa huku wengine wakidai kuwa uliharakishwa.

Miongoni mwa wale ambao walijitokeza wazi ni walimu, kupitia Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) Wilson Sossion. Kulingana naye, mapendekezo waliyotoa katika vikao vya kamati ya kuendesha mageuzi hayo hayakuzingatiwa.

Wadau wengine pia wamedai kwamba walimu waliotwikwa jukumu la kufanya majaribio yake hawakupewa mafunzo ya kutosha, huku serikali ikilaumiwa kwa kutotoa vifaa bora vya kuwafunzia.

Kimsingi, mchakato mzima ulidaiwa kukumbwa na matatizo, ila serikali ilikosa kuyazingatia katika hatua za mwanzo mwanzo. Kile kimejitokeza katika utaratibu mzima wa uahirishaji wake ni kuwa, mvutano kati ya serikali na wadau umegeuka kuwa hasara kubwa kwa wazazi na wachapishaji vitabu.

Kwa kufahamu kwamba ungeanza kutekelezwa mwaka ujao, wazazi wengi waliwanunulia wanao vitabu ili kutimiza kanuni ambazo zilikuwa zimetangazwa na wizara.

Wachapishaji vitabu nao walichapisha maelfu ya vitabu na kuyaweka madukani, ili kuhakikisha kwamba wazazi hawahangaiki kwa kuvikosa.

Wachapishaji vile vile wamejipata pabaya, baada ya baadhi ya vitabu walivyochapisha kupatikana na makosa mengi, hali inayohusishwa na kutoelewana kwa wadau kuhusu yale yaliyopaswa kujumuishwa vitabuni. Kwa haya yote, kinachojitokeza ni kwamba hali ya kutoelewana ndiyo imechangia pakubwa kutofaulu kwa hatua ya kwanza ya majaribio ya mfumo huo.

Ukosefu wa mashauriano ya kina miongoni mwa wadau wakuu pia umeuvuruga mchakato mzima hivyo kuwaacha wanafunzi, walimu na wazazi katika njiapanda.

Wito wetu ni kwamba, ikizingatiwa huu ni mfumo unaokusudiwa kutumika kwa vizazi kadhaa vijavyo, kunapaswa kuwa na mashauriano kati ya wadau wote husika.

Wadau wanapaswa kutumia muda uliopo kuuboresha mfumo huo, ili kuepuka matatizo kama haya yaliyojitokeza.