Makala

TAHARIRI: Mikakati thabiti itaokoa Shujaa

June 8th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

BAADA ya Kenya kuponea pembamba kubanduliwa katika msururu wa Raga ya Dunia ya wachezaji saba kila upande, pana haja ya Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kubuni mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa timu hii inarejea katika fahari yake ya hapo awali.

Kabla ya kuchanganua mada hii kwa kina, ni muhimu ijulikane kuwa sehemu kubwa ya masaibu yanayokumba timu hii ya taifa almaarufu Shujaa, ni ya kujitakia.

Ni ya kujitakia kwa sababu shirikisho lenyewe lilikataa kimakusudi kuwalipa vizuri au hata kuwarai wachezaji kucheza hata baada ya kuwapunguzia mishahara yao pakubwa.

Uongozi uliokuwepo ulionekana kuwapuuza wachezaji kabisa pamoja na masaibu yao hata yale ambayo yangeweza kusuluhishwa.

Kwa mfano Wizara ya Utalii ililazimika kuondoa udhamini wake wa mamilioni ya pesa mwaka jana baada ya wachezaji kukataa kutangaza Kenya katika mmojawapo wa misururu ya raga hiyo kwa kukosa kulipwa pesa walizokuwa wameahidiwa.

Japo KRU ilitoa sababu kuwa haikuwa na pesa wakati huo, swali ni je, ilikuwa imetumiaje pesa zote ilhali ilijua ina jukumu la kuwalipa mishahara na marupurupu ya wachezaji?

Kikosi cha Kenya kilikuwa kinafanya vizuri na hata kuvutia udhamini mbalimbali ikiwemo Safaricom na Kenya Airways.

Je, pesa hizo zilikuwa zikienda wapi hadi ukafika wakati ambapo shirikisho hilo likalemewa kumudu mishahara na marupurupu ya wachezaji?

Tatizo hilo lililazimu kutoweka au kufurushwa kwa wachezaji wengi wenye uzoefu wa hali ya juu; hivyo kudhoofisha timu hiyo kiasi cha kushindwa katika takribani kila mechi ya kimataifa.

Kenya haingeweza kufika robo fainali katika msururu mzima isipokuwa katika mkondo wa mwisho baada ya kung’amua kuwa ilikuwa katika hatari ya kufukuzwa.

Dawa ni gani? Jambo la kwanza ni kutafuta ufadhili kwa udi na uvumba ili tatizo la malipo liondolewe.

Pili, baada ya uongozi mpya chini ya mwenyekiti Oduor Gangla kuchukua hatamu mnamo Machi, pana haja ya kuhakikisha kuwa Shujaa inahudumiwa kwa viwango vya juu ndipo iweze kurudi ilivyokuwa.

Itakuwa bora kocha mpya mwenye ujuzi na uzoefu wa kutosha kuajiriwa. Benchi la ufundi pia lichunguzwe nao wachezaji wazoefu kama vile Willy Ambaka warejeshwe.

Mikakati thabiti ikibuniwa, Kenya itainuka na kujiondoa kwenye fedheha iliyokuwa inanukia msimu huu uliokamilika majuzi.