TAHARIRI: Miradi ya nyumba za bei nafuu ikamilishwe

TAHARIRI: Miradi ya nyumba za bei nafuu ikamilishwe

NA MHARIRI

UJENZI wa nyumba za bei nafuu kwa wananchi ilikuwa mojawapo ya ahadi kuu ambazo serikali ya Rais William Ruto ilitoa katika kampeni kabla Uchaguzi Mkuu kufanyika.

Hatua ya Rais Ruto jana Jumatatu kuzuru mradi wa ujenzi wa nyumba aina hizo katika mtaa wa Mukuru, Kaunti ya Nairobi, huenda ilikuwa imenuiwa kuashiria kujitolea kwa serikali yake kutekeleza ahadi hiyo.

Mradi wa Mukuru ni moja tu kati ya mingine mingi ambayo ilikuwa imeanzishwa katika maeneo tofauti ya nchi, mengine yakiwa kwa ushirikiano na wawekezaji wa kibinafsi.

Hatua zimepigwa katika baadhi ya miradi, lakini kuna mitaa ambapo nyumba za kale zilibomolewa ilhali ujenzi haujapiga hatua yoyote.

Ujenzi wa nyumba za bei nafuu ambazo zinaweza kununuliwa na wananchi wa matabaka ya chini, ni mpango ambao umekuwa ukijaribiwa kwa muda mrefu.

Tangu wakati wa utawala wa aliyekuwa rais, marehemu Mwai Kibaki, kumekuwa na miradi aina hii lakini changamoto mbalimbali hutokea na kuathiri utekelezaji kikamilifu.

Mojawapo ya changamoto ambazo zimekuwa sugu mno katika utekelezaji wa miradi hii ni jinsi huingiliwa kisiasa.

Katika baadhi ya miji, kuna wanasiasa ambao huchochea wakazi kupinga ubomoaji wa nyumba za jadi ili kujengwe nyumba nadhifu za kisasa zinazoweza kugawiwa idadi kubwa zaidi ya wananchi.

Hatukatai kuwa sheria na sera zote zinazolinda wananchi zinafaa kufuatwa kabla wahamishwe katika nyumba hizo za kale, lakini ni ubinafsi mkubwa kwa wanasiasa kuchochea wananchi kupinga maendeleo bila sababu.

Wananchi wanafaa kujihadhari sana dhidi ya wanasiasa wanaoonekana kujinufaisha na hali yao ya umaskini.

Badala ya kuchochea umma dhidi ya miradi aina hii, wanasiasa, hasa wabunge wana jukumu kubwa la kuhakikisha kuna sheria mwafaka za kusimamia utekelezaji mzima ikiwemo kuwahamisha wakazi kwa njia ya utu na kuhakikisha watakaonufaika na miradi hiyo ni wale wanaostahili pekee.

Hitaji la kuhakikisha wanaonufaika ni wale wanaostahili, ni jambo ambalo hasa linafaa kuchukuliwa kwa uzito.

Hii ni kutokana na kuwa, pingamizi wakati mwingi hutokea kwa msingi kuwa wale wanaoishi hapo hawana hakika kama watapata nafasi kununua nyumba hizo za bei nafuu, au kutakuwa na utapeli utakaosababisha watu wengine matajiri kumiliki nyumba karibu zote.

Ni matumaini yetu kuwa, utawala ulio mamlakani utachukulia changamoto za miaka iliyopita kama mafunzo ili kuboresha utekelezaji wa miradi hii kwa njia ambayo itanufaisha umma.

You can share this post!

Mung’aro aacha kanisa gizani kuhusu hospitali

BENSON MATHEKA: Ni makosa maafisa kama Amoth kuhudumu kama...

T L