TAHARIRI: Miungano yote ya kisiasa izingatie sera

TAHARIRI: Miungano yote ya kisiasa izingatie sera

KITENGO CHA UHARIRI

MIPANGO ya wanasiasa kuunda miungano watakayotumia katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 imeanza kushika kasi.

Kwa miezi michache ambayo imekamilika mwaka huu, kumekuwa na shughuli nyingi za wanasasa, hasa vigogo wa kisiasa ambazo zinaashiria wameanza kujiandaa vilivyo kwa kinyang’anyiro cha urais kinachotarajiwa mwaka ujao.

Kando na kiti cha urais, viongozi wa vyama vya kisiasa pia wanalenga kupata ushindi wa viti vingi katika nafasi nyingine tofauti za kisiasa ikiwemo ugavana, useneta, ubunge na udiwani.

Ilivyo desturi nchini, chama kinachofanikiwa kuwa na idadi kubwa ya viongozi katika nafasi yoyote ile huwa na ushawishi mkubwa kuhusu sera ambazo zinashughulikiwa na viongozi watakaokuwa katika ngazi hizo.

Kinachosikitisha ni kuwa, miungano mingi ya kisiasa huwa inaundwa kwa misingi ya kikabila.

Si ajabu ukikuta washauri wa wanasiasa wakipiga hesabu kuhusu idadi ya kura kutoka kwa makabila tofauti kila mara wanapoandaa mapendekezo ya uundaji wa muungano hasa utakaotumiwa kwa uwaniaji urais.

Mtindo huu wa kutumia ukabila katika siasa za nchi ni miongoni mwa vyanzo vya changamoto tele ambazo hukumba nchi hii.

Hii ni kutokana na kuwa mwelekeo huu huwafanya wananchi kupiga kura kwa misingi ya kikabila bila kujali uwezo wa wale wanaochaguliwa kuwatumikia vyema wakiwa mamlakani.

Vinara wa vyama watafanyia taifa hili jambo jema mno ikiwa watabadili mwenendo huu uliopitwa na wakati, na wajitahidi kubuni miungano kwa misingi ya sera wala sio kuzingatia wingi wa kura za makabila fulani pekee.

Kando na miungano, idadi ya vyama vya kisiasa pia inaendelea kuongezeka kadri na jinsi Uchaguzi Mkuu unavyokaribia.

Licha ya kuwa kuna sheria ya uundaji wa vyama ambayo ilinuiwa kuepusha kuwepo kwa vyama vya kisiasa vinavyosajiliwa kwa minajili ya kufaidi kifedha wanaovisajili, bado kuna vingi vinavyotiliwa shaka kuhusu nia zao.

Demokrasia ya vyama vingi haifai kutumiwa vibaya kuunda vyama vya ubinafsi au ukabila, bali kudumisha ushindani wa masuala ya sera.

Ni kupitia njia hii ambapo taifa litapiga hatua kubwa kimaendeleo kuliko jinsi ilivyo sasa.

You can share this post!

Afisa mwingine wa ODM apata Covid-19

JAMVI: Mtihani wa kuuza Muturi kama mrithi wa Uhuru Mlimani