Makala

TAHARIRI: Mivutano Jubilee ikabiliwe, haifai nchi

April 14th, 2019 1 min read

NA MHARIRI

SIASA na mivutano ya kimamlaka inayoendelea katika Chama cha Jubilee (JP) inazidi kuongezeka, kwa kiwango ambacho sasa kimeanza kuzua hofu kuhusu uthabiti wa utulivu na amani nchini.

Kila wikendi, wabunge wa mirengo ya ‘Team Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ wamekuwa wakirushiana lawama kuhusu ubabe wa kisiasa na urithi wa Rais Uhuru Kenyatta ifikapo mwaka wa 2022.

Hali hii imefikia upeo, kiasi kuwa baadhi ya wabunge wameanza kutusiana hadharani, bila kujali hadhira inayowatazama ama kuwasikiliza.

Kwa kuwa haya yote yanaendelea katika Chama cha Jubilee, ambapo kiongozi wake Rais Kenyatta, imefikia wakati ambapo inapasa aingilie kati na kudhibiti hali.

Mwelekeo huu si salama hata kidogo kwa uthabiti wa nchi, kwani baadhi ya wabunge hata wameanza kuendeleza kampeni za 2022 kiwazi, licha ya agizo la Rais kutofanya hivyo.

Katika majukwaa mengi, Rais Kenyatta amesisitiza kuwa lengo lake kuu katika muhula wake wa pili litakuwa kuiunganisha nchi, ili kupata mazingira mazuri ya kutimiza ahadi zake za maendeleo, hasa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Ni kutokana na hayo ambapo alibuni mwafaka wa kisiasa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ili kuondoa taharuki ya kisiasa iliyokuwepo nchini baada ya uchaguzi tata wa 2017.

Licha ya juhudi hizo, malumbano ya makundi hayo mawili yanatishia kuirejesha nchi pahali ilipokuwa kabla handisheki kupatikana, kwani baadhi wanaunga mkono muafaka huo na wengine wanaupinga.

Historia pevu ya jinsi ghasia hutokea nchini inaonyesha wazi kuwa mbinu kuu ambayo wanasiasa hutumia ni kuanza kujenga taharuki na chuki za kikabila.

Kwa hilo, huwa wanatumia hali hiyo kuvuruga uthabiti wa kisiasa ambao huwepo kujitakasa, huku wakiwalaumu washindani wao kwa athari ambazo baadaye hutokea.

Kama kiongozi wa nchi na Jubilee, Rais Kenyatta ana mamlaka ya kumwadhibu mwanachama yeyote ambaye anakiuka taratibu zilizowekwa.

Si mara moja ametoa maagizo na onyo kwa wabunge kukoma kujenga taharuki zisizofaa.Imefikia wakati ambapo anapaswa kudhihirisha mamlaka yake kwa kuchukua hatua zinazofaa.