TAHARIRI: Msimamo wa Cotu ni machozi ya mamba

TAHARIRI: Msimamo wa Cotu ni machozi ya mamba

KITENGO CHA UHARIRI

MUUNGANO wa vyama vya kutetea haki za wafanyakazi (COTU) umetoa kauli ya kupinga kuongezwa kwa kodi inayotozwa wafanyikazi wanapokea mishahara ya kuanzia Sh32,333.

Chama hicho kinaitaka wizara ya Hazina ibuni njia mbadala ya kuinua fedha za kuendeleza uchumi, badala ya kuwabebesha wafanyikazi mzigo zaidi kupitia ushuru wa juu.

Muungano huu wa vyama umeishauri mamlaka ya ushuru nchini (KRA) ibuni mikakati mpya ya kuwaandama Wakenya ambao wameshamiri katika mbinu za kukwepa ulipaji kodi walipe.

Kulingana na Cotu, ni kwa KRA kuwatoza wafanyakazi viwango vya juu vya kodi na tayari wameathiriwa zaidi na makali ya mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19.

Msimamo huo wa Cotu uko sahihi. Serikali haifai kuwatoza wafanyikazi kodi zaidi, kwa vile wanaendelea kuumia kutokana na janga la ugonjwa wa Corona.

Si wafanyikazi wa kiwango cha chini pekee wanaoumizwa na baadhi ya sera mpya zilizoanza kutumika kuanzia Januari mosi. Wafanyibiashara wengi waliumia wakati wa kufungwa kwa nchi kutokana na kusambaa kwa Corona mwanzoni mwa mwaka jana.

Kufikia sasa, watu hawawezi kuendeleza biashara zao saa 24 kama ilivyokuwa kabla ya marufuku ya watu kutoka nje nyakati za usiku. Cha kushangaza ni kuwa, kila kitu kimeanza kurejelea hali ya kawaida kwa upande wa serikali.

Kampuni nyingi bado zinakabiliana na hali ngumu ya kiuchumi. Kutokana na kukosekana fedha, wakuu wa baadhi ya kampuni wameendelea kukwamilia mishahara ya wafanyikazi. Wale waliopata afueni kidogo wameanza kuwarejeshea asilimia kidogo.

Lakini serikali kufikia Januari 1, iliwaondolea afueni wafanyikazi wote na kudai kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kujiondoa kutoka kwa hali ngumu inayoikumba.

Sheria iliyorejesha ushuru palipo ulipokuwa kabla ya Aprili mwaka jana, ilipendekezwa na waziri wa Fedha Ukur Yattani tangu mwezi wa Oktoba mwaka jana. Baadaye mswada ukachapishwa na kujadiliwa bungeni. Hata ulipopita, ulichukua siku kadhaa kabla ya Rais kuutia saini na kuwa sheria.

Kama kweli Cotu ilikuwa inapinga kurejeshwa kwa ushuru kamili kabla wafanyikazi na Wakenya kwa jumla hawajapata afueni, ingefanya hivyo mapema. Kututangazia sasa kwamba hatua hiyo haifai kuhadaa ulimwengu. Hicho ni kilio cha machozi ya mamba.

You can share this post!

JAMVI: Mikosi ya usaliti kwa miungano ya kisiasa uchaguzi...

Guardiola kuwa kocha kwa muda mrefu zaidi kuliko jinsi...