Makala

TAHARIRI: Mti gani utapevuka kwa miezi mitatu?

February 26th, 2018 2 min read

Naibu Rais Bw William Ruto. Ameweka marufuku ya siku 90 dhidi ya ukataji wa miti nchini. Picha/ Maktaba

Na MHARIRI

SERIKALI imepiga marufuku ukataji wa miti katika misitu yote nchini, iwe ni ya kitaifa au ya kijamii.

Katika kipindi cha siku 90, Wizara ya Mazingira na Misitu itahitajika kushauriana na wadau wote ili kubuni jopo kazi la kufanyia misitu utathmini, na kuchapisha ripoti baada ya siku 14 kutoa mapendekezo kuhusu hatua zinazofaa kuchukuliwa kuokoa mazingira ya Kenya.

Amri hiyo ya kisheria ilitolewa wikendi na Naibu Rais William Ruto, wakati ambapo athari ya kiangazi inazidi kushuhudiwa katika maeneo tofauti nchini.

Kulingana na Bw Ruto, kiangazi kikali ambacho kimeshuhudiwa kwa karibu miaka mitatu sasa kimesababisha uhaba wa maji mitoni na katika chemchemi za maji.

Naibu Rais anaamini hali hii imetokana na ukataji wa miti kiholela pamoja na jinsi watu wanavyonyakua maeneo yanayotega maji, jambo ambalo limeathiri vibaya uwezo wa nchi kuzalisha chakula cha kutosheleza mahitaji ya umma.

Ukataji wa miti misituni umekuwa ukishuhudiwa sana kutokana na unyakuzi wa ardhi zilizotengwa kuwa misitu, mbali na biashara za mbao, uchomaji wa makaa na jinsi jamii mbalimbali zinavyojenga vijiji vyao misituni.

Miongoni mwa misitu ambayo imeathirika zaidi na ukataji wa miti kiholela ni msitu wa Mau ambao unategemewa kutega maji yanayoingia mito ya Ewaso Ng’iro Kusini, Sondu, Mara na Njoro. Mito hii hupeleka maji kwa maziwa makubwa ya Victoria, Nakuru na Natron.

Mbali na msitu wa Mau, misitu mingine katika maeneo tofauti nchini pia yamekuwa yakiharibiwa kama vile msitu wa Ngong ulio Kaunti ya Nairobi.

Japokuwa nia ya hatua hiyo ni nzuri, inaonekana amri hiyo ilitolewa bila ya kuzingatia mambo ya msingi. Kama lengo ni kuwa na miti ya kutosha, miezi mitatu itasaidia vipi? Wakati huu wa kiangazi, miti mipya itapandwa kutumia maji gani? Je, itapevuka katika muda huo?

Serikali pia haijaweka mikakati ya kisheria wala kuhusisha wadau kama ilivyokuwa wakati wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki.

Kwa sababu hiyo, kuna haja ya kufikiria upya na kuwashirikisha wadau wengine, ili mpango huo usiwe ni wa siku 90 pekee, bali utakaoiwezesha nchi kufikia angalau asilimia 10 ya misitu.