Makala

TAHARIRI: Mvua iwe baraka kwa hatua zifaazo

March 12th, 2018 2 min read

Na MHARIRI

MVUA inatarajiwa kuanza Jumatatu katika maeneo mengi ya nchi, siku chache tu baada ya nyingine iliyonyesha kwa juma moja kutulia.

Habari hizi ni za kutia moyo ikizingatiwa ukame wa muda mrefu ulioshuhudiwa nchini. Kiangazi hiki kilisababisha matatizo mengi kama vile njaa, uhaba wa maji na kudidimia kwa shughuli za kiuchumi.

Kwa hivyo ujio wa mvua ni afueni kubwa kwa taifa lote ikizingatiwa kuwa sasa wakulima watakuwa na fursa ya kuzalisha mazao, uhaba wa maji na chakula kupungua na mengine mengi.

Lakini katika tangazo lake kuhusu mvua hii, Idara ya Anga ilitoa tahadhari ya mafuriko kushuhudiwa katika sehemu kadhaa nchini kutokana na mvua hiyo. Hali ya mafuriko ilishuhudiwa wiki iliyopita ambapo watu kadhaa walipoteza maisha na mali ya thamani kubwa kuharibiwa.

Kila mara kabla ya mvua kubwa kunyesha, idara hii imekuwa ikitoa tahadhari za mafuriko pamoja na magonjwa. Mvua hunyesha, inasababisha hasara, watu wanakufa kisha inakoma. Baada ya wiki kadhaa madhara yake husahauliwa.

Inafaa kukumbuka kuwa kila jambo lina manufaa yake na pia hasara iwapo halitathibitiwa. Mvua ni baraka lakini inaweza kuwa hasara iwapo hatutachukua hatua za kuthibiti makali yake.

Katika miji kama vile Nairobi, Mombasa na Narok kumeshuhudiwa mafuriko mitaani na barabarani kwa miaka mingi. Lakini inaoenekana wasimamizi wa miji hii hawana nia ya kuepusha wakazi kutokana na madhara ya mafuriko.

Inafahamika wazi kuwa mafuriko husababishwa na miundo duni ya kupitisha maji na taka, ujenzi katika maeneo yasiyostahili, ujenzi mbovu wa barabara miongoni mwa mengine ambayo yanaweza kuepushwa.

Maafisa wa miji hii huwa hawachukui hatua zozote za kuzuia majanga yanayotokana na maji kama vile kuzimbua mitaro ya maji na kuhakikisha sheria za ujenzi zinafuatwa na wote bila kujali vyeo vyao.

Ni jambo la kusikitisha kuwa waliopewa majukumu ya kuhakikisha wakazi wa miji husika wanaishi katika mazingira salama iwe mvua ama jua hawajishughulishi.

Magavana wa kaunti mbalimbali wana jukumu la kuhakikisha kuwa maafisa wanaosimamia miji wanatekeleza majukumu yao kikamilifu ili kulinda maisha na mali ya wakazi.