Makala

TAHARIRI: Mzigo wa ushuru usiachiwe wachache

October 22nd, 2018 2 min read

NA MHARIRI

KENYA imeshindwa kufikia matarajio yake ya ukusanyaji ushuru kutokana na kuendelea kutegemea sekta chache za kiuchumi kulipa ushuru.

Kwa miaka mingi watu walioajiriwa rasmi ndio wamekuwa wakibebeshwa mzigo wa kulipa ushuru kutokana na sababu kwamba ni rahisi kwa Mamlaka ya Ushuru (KRA) kuchukua ushuru kutoka kwao kupitia kwa waajiri. Hatua hii imefanya watu walio katika ajira kunyanyaswa kwa muda mrefu na mwishowe kuenda nyumbani na mshahara kidogo.

Wataalamu wa uchumi wanakiri kuwa unapotoza idadi ndogo ya watu ushuru unaishia kuwatoza kiwango cha juu cha kodi na hivyo kuwakandamiza.

Hii ni licha ya kuwa walio katika sekta ya Jua Kali wanaingiza mapato ya juu ambayo hayatwozwi ushuru ama iwapo wanalipa unakuwa ni wa chini ikilinganishwa na watu walio kwenye ajira ya serikali.

Makosa mengine ambayo yanafanya Kenya ishindwe kufikia shabaha yake ya ushuru ni kuwapendelea watu wa ngazi za juu serikalini kwa kuwapunguzia ushuru wanaopasa kulipa.

Aidha, ushuru unaotozwa wafanyabiashara na wawekezaji wengine ndio umekuwa sababu ya Kenya kuonekana kuwa mahali pasipo na mazingira bora ya uwekezaji. Ni sababu kama hizi ndizo zimekuwa zikiwafanya baadhi ya wawekezaji kufunga biashara zao nchini na kutorokea mataifa mengine jirani yetu.

Ili Serikali iweze kupata pesa za kutosha kugharimia miradi yake, ni sharti ipanue nyavu zake za kutoza ushuru ili kila mtu aliye na pato la namna yoyote achangie katika jungu la kodi.

Kwa kufanya hivyo, kutakuwa na idadi kubwa ya watu wanaolipa ushuru, hatua ambayo itaweza kusaidia kupunguza viwango vya kodi inayotozwa Wakenya kwa sababu haitakuwa kama sasa ambapo watu wachache ndio wanaotegemewa.

Hatua ya namna hii pia itasaidia nchi kuwa na pesa za kutosha kugharimia miradi ya maendeleo na hatimaye kuweza kusaidia kupunguza ukopaji ambao kwa sasa umeweka Kenya katika njia panda.

Ni sharti KRA na Wizara ya Fedha zibuni njia mwafaka za kuhakikisha kwamba idadi ya walipa ushuru imeongezeka ili kumaliza mtazamo finyu wa kutoza zaidi watu wachache huku walio wengi wakiachwa.