Makala

TAHARIRI: Mzozo wa Knut usitatize masomo

August 30th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

MZOZO wa uongozi unaokumba chama cha walimu cha Knut ni hatari kwa elimu nchini hasa wakati shule zinatarajiwa kufunguliwa wiki ijayo.

Ni wazi kuwa mzozo huo umegawanya walimu ambao ndio wanachama wa chama hicho na ambao wanatarajiwa kuandaa wanafunzi katika muhula wa tatu mwaka huu hasa wanaofanya mitihani ya kitaifa.

Hofu yetu ni kuwa kwa sababu chama hicho hutetea maslahi ya walimu, wanaweza kutumia muda mwingi wakijadili mzozo wa uongozi wake na kuathiri masomo.

Tayari mzozo huo umeathiri baadhi ya walimu ambao walikosa kuongezewa mshahara.

Hii ni hatua inayoweza kushusha motisha wa walimu hao na hivyo kuathiri maandalizi ya mitihani na masomo kwa jumula.

Muhula wa tatu huwa ni muhimu sana kwa wanafunzi katika kalenda ya elimu Kenya kwa sababu mbali na mitihani ya kitaifa, wanafunzi huwa wanajiandaa kuingia darasa au kidato kinachofuatia.

Hatua yoyote inayoathiri maandalizi hayo huwa inaathiri sio tu masomo yao mbali pia saikolojia yao. Knut inafaa kutatua mzozo wao wakijua kwamba walimu wana jukumu kufanikisha masomo nchini na mwajiri wao anaweza kutumia mzozo huo kuadhibu walimu watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Ukiwa wakati ambao mtaala wa elimu unafanyiwa mageuzi, walimu hawafai kuhusika na hatua yoyote inayoweza kuathiri ratiba iliyowekwa kufanisha mtaala mpya.

Walimu wanapaswa kufahamu kuwa mwajiri wao anatazama na kufuatilia matukio katika chama chao na wale ambao watashawishika kususia kazi wanaweza kujipata pabaya.

Ukweli wa mambo ni kuwa mvutano katika Knut utaathiri walimu zaidi ikiwa utaendelea na wanafunzi hawatasazwa. Wakiwa wazazi, viongozi wa Knut wanapaswa kuelewa uchungu wa masomo ya wanafunzi kuathiriwa na mizozo isiyowahusu.

Wazazi huwa wanawekeza pesa nyingi ili watoto wao wapate elimu na inauma kuona walimu wenyewe wakizozana.

Ni matumaini yetu kwamba pande zote zinazovutana zitajali maslahi ya wanafunzi wanaofanya mitihani na ambao wanahitaji kushughulikiwa kwa umakini.

Itakuwa vibaya tamaa ya uongozi ya watu wachache kuathiri maelfu ya wanafunzi na sekta ya elimu nchini.