Makala

TAHARIRI: Naam, wanafunzi 150,000 watafutwe waliko

February 7th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

HATUA ya serikali kuahidi kufuatilia waliko wanafunzi wanaozidi 150,000 waliokosa kujiunga na shule za upili inafaa zaidi kwani ni muhimu kufahamu ni sababu zipi zilizowazuia watoto hao kuendeleza masomo yao ya sekondari.

Kati ya wanafunzi wapatao milioni moja waliofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) mwaka jana, ni takribani laki nane pekee waliojiunga na sekondari huku wengine wakikosa kujilikana waliko.

Hata hivyo, sababu kuu ya kutojiunga na shule za sekondari kwa wengi wao inaweza kujulikana kwa urahisi. Yakini wengi wao wameshindwa kujiunga na shule za upili kutokana na ukosefu wa karo. Japo serikali imeeleza kuwa imefadhili masomo ya wanafunzi wa kutwa katika shule za sekondari, ukweli ni kwamba bado shule zinatoza karo ya juu ambayo wengi wa wazazi hawawezi kumudu.

Kutokana na ugumu wa maisha, wazazi wengi hushindwa kupata pesa hizo na hivyo basi kuamua ama kuwapeleka watoto wao kusaka vibarua au kujifunza kazi za juakali ili waweze kumudu maisha yao.

Japo tunatia shime serikali iandame azma yake ya kufuatilia waliko watoto hao, itakuwa bora itafute mkakati wa kuhakikisha wazazi wote maskini wameweza kuwapeleka watoto wao katika shule za upili.

Cha kukatisha tamaa hata zaidi ni kwamba baadhi ya watoto hao, ni werevu hivyo basi akili zao zote zinaenda kudumaa kutokana na tatizo la ukosefu wa fedha.

Itakuwa bora serikali ihakikishe kuwa masomo ya shule za upili ni ya bure kote nchini ili kuweza kukabiliana na tatizo hili. Hamna haja ya serikali kusema kuwa inadhamini masomo ya wanafunzi, hasa wa kutwa ilhali wengi wanakosa kuendeleza masomo yao kutokana na ukosefu wa pesa.

Shule za sekondari hususan zile za daraja za chini zafaa zilazimishwe kutotoza wanafunzi pesa zozote maadamu zile zinazotolewa na serikali zinatosha kugharimia mahitaji yote muhimu ya wanafunzi hao wawapo shuleni.

Serikali hutoa Sh22,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka. Pesa hizo kwa hakika zinatosha kugharimia kila hitaji la mwanafunzi wa kutwa ikiwemo chakula, ada ya ujenzi na gharama nyingine mbalimbali shuleni. Hivyo basi haipo sababu ya wazazi kuendelea kutwikwa mzigo wa ziada wa kulipa karo.