TAHARIRI: Ni msimu wa Krismasi kila mmoja awe mwangalifu

TAHARIRI: Ni msimu wa Krismasi kila mmoja awe mwangalifu

KITENGO cha UHARIRI

SHAMRASHAMRA za Krismasi na Mwaka Mpya zinapobisha hodi duniani kote, kila mmoja wetu huwa na matumaini makubwa kufikia na kuvuka tarehe hiyo akiwa mzima, hai na buheri wa afya kiasi cha kujumuika pamoja na jamaa marafiki zake kufurahia pamoja.

Hata hivyo, inakuwa ni huzuni isiyo na kifani ikiwa mmoja atapoteza jamaa au hata rafiki kipindi hiki cha sherehe. Takwimu za mwezi wa Novemba zinaonyesha kwamba idadi kubwa ya ajali ilishuhudiwa mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Kulingana na Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna watu 4.023 walipoteza maisha yao kupitia ajali ikilinganishwa na 3.340 mwaka jana. Ripoti hii inafichua kwamba wanaochangia ajali hizi zaidi ni waendeshaji pikipiki, wapitanjia au watembeaji, abiria na madereva kwa mpangilio huo.

Ni wazi kwamba idadi ya ajali hupanda kila mwezi wa Desemba hasa msimu wa sherehe. Hii hutokana na hali ya kutojali kwa wengi wanapojiingiza kwa starehe na anasa kuadhimisha Sikukuu hii ya mara moja kwa mwaka.Tayari habari za tanzia, huzuni, majonzi na masikitiko zimeanza kuhanikiza kote nchini kufuatia mauti yaliyoshuhudiwa maeneo ya Mwingi, Kaunti ya Kitui na Bondo, Kaunti ya Siaya.

Hili ni ishara kuwa tusipotahadhari huenda mwezi huu ukawa mbaya zaidi.Ili kujiepusha na misiba wakati wa sherehe ni sharti kila mmoja wetu awe makini kuepuka ghadhabu za wadereva na waendesha pikipiki.Madereva wa magari ya umma na ya kibinafsi wazingatie kanuni za trafiki.

Mwendo wa kasi ni hatari kwa maisha ya abiria. Madereva wasiendeshe magari wakiwa walevi. Utafiti umeafiki kwamba ajali nyingi zinazotokea msimu wa Sikukuu husababishwa na tabia za ulevi na kutokujali kwingi.Abiria wana jukumu la kulinda maisha yao dhidi ya magari mabovu au madereva wasio na nidhamu.

Wasikubali kuabiri magari yaliyobeba kupita kiasi au wanayoendeshwa na watundu. Tahadhari zaidi zinafaa kuchukuliwa na wahudumu wa bodaboda ambao kwa sasa ndio wanaongoza orodha ya wanaosababisha ajali nchini. Tume ya Huduma ya Polisi Nchini (NPC) ikishirikiana na Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Nchini (NTSA) kuhakikisha bodaboda wote wana leseni na nidhamu barabarani.

Maafisa wa polisi wasikubali kuchukua hongo kufunika kosa la yeyote. Mvua huchangia pia kwenye ajali kwani barabara huwa telezi. Hili litiliwe maanani. Tusikubali kusombwa na maji au kugongwa na gari. Tujilinde sisi pamoja na wapendwa wetu. Tutahadhari kabla ya athari.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Ushirikiano wahitajika kuzuia ajali msimu...

Jeshi lamhukumu Suu Kyi miaka 4 gerezani

T L