Makala

TAHARIRI: Ni unafiki mkuu kumlaumu waziri kwa mimba za mapema

November 7th, 2018 2 min read

NA MHARIRI

BAADHI ya viongozi wa kisiasa wamejitokeza kulaumu Wizara ya Elimu kwa mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi, hatua ambayo haifai.

Japo Wizara ya Elimu inapaswa kuweka sera mahsusi kuhakikisha mimba za mapema shuleni zimekabiliwa, jukumu kubwa la kuzima visa hivyo ni kwa wazazi na jamii kwa jumla.

Mamia ya wanafunzi wamefanyia mitihani ya kitaifa katika hospitali baada ya kujifungua huku wengine wakitoroka ili kuolewa baada ya kupachikwa mimba.

Huu ni mtindo ambao unahatarisha mustakabali wa kizazi kijacho na sharti viongozi wote husika waungane kupata suluhu ya kudumu bila kulaumiana.

Jana, Mbunge wa Cherang’any Joshua Kuttuny pamoja na Seneta wa Kaunti ya Nandi(Samson Cherargei) walimnyooshea kidole cha lawama Waziri wa Elimu Amina Mohamed na maafisa wake kwa kushindwa kuweka sera za kuzuia wanafunzi kupata mimba wakiwa shuleni.

Viongozi hao walimtaka Bi Mohamed kuwajibika na kuhakikisha wanafunzi wanalindwa kutokana na uhalifu huo.

Wanasiasa hao wamekosa kufahamu kuwa wanafunzi wengi wanapachikwa mimba wakati wa likizo hivyo hawafai kushutumu wizara ya elimu kwa uozo huo.

Wazazi, ambao wanajumuisha wabunge hao, wana jukumu la kwanza kuhakikisha wanawadhibiti watoto wao wakati wako likizoni.

Itakuwa vigumu kwa Wizara ya Elimu kufuatilia maisha ya wanafunzi wakiwa nyumbani ili kuzima mimba za mapema.

Wabunge wakome kujifanya kuwa hawana jukumu katika suala hili kwani wao ndio wanaotunga sheria ambazo zinapaswa kusaidia kukomesha uhalifu huu.

Kwa mfano, wabunge wanapaswa kubadilisha Sheria ya Dhuluma za Kimapenzi kuhakikisha washukiwa wanaachiliwa kwa kiasi kikubwa cha bondi badala ya Sh100,000 ya sasa.

Vilevile, kupitia sheria mpya, Bunge lina uwezo wa kuhakikisha wazazi wanaochangia watoto wao kudungwa mimba wakiwa umri mdogo wamekabiliwa na kuadhibiwa kisheria.

Cha mno hapa ni kila mhusika kuwajibika ili lengo kuu liwe kunasua wasichana wadogo mikononi mwa wahalifu ambao wako miongoni mwa jamii.

Bw Kuttuny na wenzake wanapaswa kushirikiana na Bi Mohamed kuhakikisha sheria za kuzima visa hivyo zimewekwa na utekelezaji wake unazingatiwa kikamilifu.