Makala

TAHARIRI: Ni wazi hatua za ugatuzi bado hafifu

March 7th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

KONGAMANO la siku tatu la Ugatuzi lilimalizika katika Kaunti ya Kirinyaga Alhamisi huku mambo kadha wa kadha yakijitokeza.

La kwanza na ambalo limekuwa kawaida kwa mikutano yoyote iliyo na hadhara ni kwamba siasa zilishamiri haswa majibizano baina ya Naibu Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga kuhusu ufisadi.

Bw Odinga alipomshambulia Bw Ruto Jumatano kuhusu kiasi kamili cha fedha zilizonuiwa kujenga mabwawa eneo la Elgeyo Marakwet na haswa alipomtaka Naibu Rais huyo aeleze alivyofahamu bayana sio Sh21 bilioni zilizoibwa bali ni Sh7 bilioni, Bw Ruto alichukua nafasi wakati wa kufunga kongamano hilo Alhamisi kumsuta Bw Odinga na kumwita kizingiti chenyewe katika vita dhidi ya ufisadi.

Lakini itakuwa rahisi sana kusahau mengi yaliyotendekea katika kongamano nzima na kukumbuka pekee ‘masumbwi’ haya ya kisiasa baina ya watani wa muda mrefu.

Kile ambacho kilinasa macho ya wadadisi na waangalizi wa yaliyojiri kwenye kongamano hilo la sita kufanyika tangu Ugatuzi uanze ni jinsi hali duni ilivyodhihirika katika kaunti zetu.

Kila wakati watu wanapozungumzia kuhusu Ugatuzi, huzungumza kwa maneno ya kusisimua na kuibua taswira kwamba kama taifa tunapiga hatua kubwa.

Lakini kilichoshuhudiwa Kirinyaga, kwenye hema ambazo kila kaunti iliweka kuonyesha bidhaa na mazao yanayozalishwa kwenye kaunti zao kilivunja moyo pakubwa.

Kweli kaunti kadhaa zilionyesha ubunifu wa kiteknolojia kupitia bidhaa na huduma walizoonyesha kutoa, mfano ukiwa Kaunti ya Kirinyaga iliyoonyesha nguo za shule zinazoundwa huko, nayo Makueni ikionyesha bidhaa za maziwa na sharubati zinazotokana na mazao ya wakulima wa eneo hilo, kaunti zingine hata hivyo ziliishia kuonyesha vitu kama changarawe, mapambo na vikapu vya kawaida vilivyoibua ukosoaji miongoni mwa wa wanajamii mitandaoni.

Haiwezekani kwamba mabilioni ya pesa yanayotumwa kwa kaunti kila mwaka wa kifedha yameweza kufanikisha kiwango duni cha maendeleo namna hiyo.

Wakati ambapo wakulima wanalia kwa kukosa kwa kupeleka mazao yao wakati wa msimu wa mavuno, huku ubunifu wa hali ya juu ukidhihirika miongoni mwa vijana ambao wanatafuta mwanya wa kuzalisha bidhaa za hali ya juu na walichokosa pekee ni ufadhili wa serikali zilizo karibu nao, inasikitisha kwamba bado matunda yaliyosubiriwa kupatikana kutoka kwa ugatuzi yangali mabichi miaka sita baadaye.