TAHARIRI: Njaa haifai kusumbua miaka 58 tangu uhuru

TAHARIRI: Njaa haifai kusumbua miaka 58 tangu uhuru

KITENGO cha UHARIRI

KENYA ilipojipatia uhuru wake, waasisi wa nchi hii walitangaza vita dhidi ya maadui wanne: ujinga, umaskini, maradhi na njaa.

Miaka 58 baadaye, hatua kubwa zimepigwa katika kupambana na maadui watatu; ujinga, umaskini na maradhi.Elimu ni lazima kwa kila mtoto. Mnamo 2013, masomo ya shule ya msingi yalianza kutolewa bila malipo. Karo ya shule za sekondari za kutwa imeondolewa na wanafunzi wanalipa kiasi kidogo tu cha fedha za chakula cha mchana.

Wanafunzi wote wanaokamilisha elimu ya msingi wanajiunga na sekondari na idadi ya wanaohitimu elimu ya vyuo vikuu imeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miongo mitatu iliyopita.Serikali pia imejaribu kwa kiwango kikubwa kupambana na umaskini japo mengi yanahitajika kufanywa kwa kuweka mazingira mwafaka yatakayowezesha mamilioni ya Wakenya kupata kazi.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi nchini, huduma za matibabu zimeimarika kote nchini japo gharama ya kutibu baadhi ya maradhi kama vile kansa, iko juu.Lakini inaonekana baa la njaa limesalia donda sugu nchini. Huku leo tukiadhimisha miaka 58 tangu Kenya kutangazwa jamhuri, mamilioni ya Wakenya hawajui jioni watalisha watoto wao nini kutokana na ukosefu wa chakula!

Mnamo Septemba, mwaka huu, Rais Kenyatta alitangaza ukame kuwa janga la kitaifa. Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa zaidi ya Wakenya milioni 2.3, haswa katika kaunti 23, wanahitaji chakula kwa dharura.Njaa imekuwa donda sugu humu nchini kwani imekuwa ikihangaisha mamilioni ya Wakenya kila mwaka.

Katika hotuba yake ya Disemba 12, 2014, Rais Kenyatta aliahidi kuanzishwa kwa mradi wa unyunyiziaji maji wa ekari 1,000,000 katika eneo la Galana-Kulalu kuongeza uzalishaji wa mlo. Kulingana na Rais Kenyatta, iwapo mradi huo ungekamilika, janga la njaa nchini Kenya lingezikwa katika kaburi la sahau na Kenya ingelisha nchi za Afrika na ulimwengu.

Lakini miaka saba baadaye, Wakenya hawajaona matunda ya mradi huo na njaa inaendelea kukeketa Wakenya. Kenya inalazimika kununua chakula kutoka kwa mataifa jirani ili kulisha watu wake.Rais Kenyatta anaweza kutumia miezi minane iliyosalia kabla ya kuondoka mamlakani kuelekeza nguvu zake katika uboreshaji wa kilimo.

You can share this post!

Amri mzee, 76, asiuze nyumba ya jamaa yake

Mwiraria: Waziri stadi na mweledi wa uchumi

T L