TAHARIRI: Njia za kujiondoa kutoka muungano wa kisiasa zi wazi, UDM wazifuate

TAHARIRI: Njia za kujiondoa kutoka muungano wa kisiasa zi wazi, UDM wazifuate

NA MHARIRI

KELELE zinazoendelea kusikika kutoka kwa wanasiasa wa chama cha United Democratic Movement (UDM) kuhusu kujiondoa kutoka kwa muungano wa Azimio One Kenya zinaudhi.

Kinara wa chama hicho, Seneta Ali Roba na mbunge wa Lunga Lunga Mangale Chiforomondo, wanaongoza kelele hizi huku Bw Chiforomondo akienda mahakamani.

Lengo la tahariri hii si kuzungumzia kesi yake, bali kutaka wanasiasa hao na wenzao waliokiuka sheria, kuanza kibarua walichopewa na wapigakura mnamo Agosti 9, 2022.

Bw Roba na Choforomondo wanapaswa kujua kwamba wakazi wa Mandera na Lunga Lunga waliwachagua kwa misingi miwili; kwanza kwa kuwa walikuwa mrengo wa Azimio, na pili ili wawafanyie kazi.

Wakati wa uchaguzi huo kulikuwa na wanasiasa wengi maarufu kuliko wawili hao katika maeneo yao, lakini wananchi waliwachagua wakiwa na matumaini watatekeleza ahadi walizotoa kwenye kampeni.

Watu wa Lunga Lunga walikuwa na hiari ya kuchagua mwaniaji wa Kenya Kwanza, mbunge wa zamani Khatibu Mwashetani, lakini hawakufanya hivyo.

Ni madharau kwake kuamua kwamba waliompigia kura ni wapumbavu.

Bw Roba pia anajua vyema kwamba yeye si mwanasiasa pekee aliyesimama kwenye kiti cha useneta Mandera.

Kutumia vifungu vya 37 na 38 vya Katiba kwamba kila mtu ana uhuru wa kujihusisha na upande atakao na kufanya maamuzi ya kisiasa mtawalia, ni kuelewa vibaya sheria.

UDM ilipoamua kuandikiana mkataba na Azimio One Kenya, tayari ilitimiza vifungu hivyo.

Kama ni kweli kuwa Bw Roba alitia saini mkataba bila kuusoma, atakuwa anaonyesha mfano gani kwa mwananchi wa Mandera asiyejua kusoma wala kuandika?

Sehemu ya 7(9) ya Sheria ya Vyama vya Siasa mwaka 2022 inasema kuwa mtu hawezi kuwa kwenye miungano miwili ya kisiasa wakati mmoja.

Kama vyama vya Pamoja African Alliance (PAA) na Maendeleo Chapchap vilijiunga na Kenya Kwanza kimatendo, haina maana kuwa viko ndani ya muungano huo.

Mkataba waliouweka kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa uko wazi kuwa wanaweza kujitoa baada ya miezi 3 kutoka siku ya uchaguzi. Hata hivyo, ni sharti kwanza UDM iwasilishe notisi kwa Baraza la Azimio. Ndio maana korti ilikataa ombi la PAA na Maendeleo Chap Chap.

Kama ni lazima UDM iondoke Azimio, ifanye hivyo kimya kimya kwa kufuata sheria za nchi, wala si kupiga kelele.Bw Roba anapaswa ashughulikie tatizo la njaa inayowakumba watu wa Mandera na maeneo mengine kame, badala ya kupoteza muda katika suala lililo wazi kisheria.

You can share this post!

Kufutwa kazi Kulundu kwakera Azimio

Mbappe afokewa vikali na wafuasi wa PSG

T L