Makala

TAHARIRI: Nuru ya Krismasi ni kuwajali wengine

December 25th, 2020 2 min read

NA MHARIRI

KWA mara nyingine Mwenyezi Mungu ametufikisha siku ya leo, ambayo waumini wa dini ya Ukristo kote ulimwenguni wanaungana kwa sherehe ya Krismasi.

Hii ni siku ambapo waumini hao huungana na kukumbuka huruma na mafunzo ya Yesu kuhusu kuwajali wajane, mayatima, wanawake kati ya wengine wasiobahatika katika jamii.

Ni siku inayotumika zaidi kuzileta pamoja familia, na kuwakutanisha watu ambao huenda hawajaonana kwa kipindi kirefu.Humu nchini, kuna wale ambao walifanikiwa kwenda kuisherehekea siku hii kwao mashambani.

Kwa waliobakia mijini, huu pia ni muda wa kuwajulia hali marafiki na majirani, hasa wakati huu ambapo familia nyingi zimekumbwa na athari za ugonjwa wa corona.Kutangamana wakati huu kwafaa kufanywa kwa njia ya kuzingatia kanuni zilizowekwa na wizara ya Afya.

Ingawa ni siku ya watu kufurahi na kujumuika kwenye maeneo ya burudani baadaye jioni, yatupasa tukumbuke ushauri wa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kwamba tunaishi katika nyakati zisizokuwa za kawaida.

Kwamba iwapo tutauchukulia ugonjwa huu kuwa wa kawaida, basi utatuonyesha vituko visivyo vya kawaida.Kufikia jana, nchi ilikuwa imerekodi jumla ya visa 95,431 vya watu walioambukizwa corona na wengine 1,652 wamefariki dunia.

Sikukuu hii inajiri wakati ambapo kuna wimbi jipya la maambukizi ya corona, hata katika mataifa yanayosema yamevumbua chanjo yake. Corona hiyo mpya ni hatari na inayoangamiza kwa kasi.

Wakati kama huu mara nyingi huwa tunasikia habari za ajali barabarani kutokana na watu wanaolewa chakari lakini wakataka kuendesha magari au kuvuka barabara.

Polisi wa trafiki na maafisa wa Mamlaka ya Uchukuzi na Kudhibiti Usalama Barabarani (NTSA), wana jukumu la kusaidia watu kama hao kukaa mbali na barabara kwa kuwakamata na kuwazuilia hadi watakaporudiwa na fahamu.

Muhimu zaidi wakati huu wa sherehe za leo na baadae za Mwaka Mpya, ni kutambua kuwa hata kukiwa na hali ngumu ya maisha, majukumu ya Januari bado yanatusubiri.

Watu wajiburudishe kwa kipimo, wakifahamu kwamba kuna mahitaji mengine muhimu baada ya leo. Tusherehekee Krismasi kwa nidhamu na kuwajali wenzetu.