TAHARIRI: Ongezeko la ajali linatia wasiwasi

TAHARIRI: Ongezeko la ajali linatia wasiwasi

KITENGO CHA UHARIRI

AJALI zilizosababisha vifo vya watu 18 maeneo tofauti nchini zinatia wasiwasi hasa wakati huu ambao wanafunzi wanajiandaa kusafiri kurudi shuleni kwa muhula wa tatu.

Inasikitisha kwamba zaidi ya watu 20 walifariki katika siku tatu kwenye ajali barabarani.

Hawa ni ndugu, jamaa na marafiki wa watu walioangamizwa na madereva wasiozingatia sheria za barabarani.

Madereva hawafai kukumbushwa umuhimu wa kuwa waangalifu barabarani. Inasikitisha kwamba ajali hizi zimeanza kuongezeka wiki moja baada ya masharti ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona kulegezwa, na siku tatu kabla ya kufunguliwa kwa shule.

Hii pamoja na kwamba janga la corona bado ni tishio kwa maisha ya wengi inaonyesha kuwa idara zinazohusika zimeanza kulegeza kamba katika kutekeleza sheria za barabarani.Madereva wenye tamaa ya pesa wanaendesha magari kwa kasi, wakiwa walevi baada ya vilabu kufunguliwa na saa za kafyu kupunguzwa kutoka saa mbili usiku hadi saa nne usiku. Hii inawapa muda wa kuketi vilabuni kulewa.

Mwendo wa kasi, madereva kuendesha magari wakiwa walevi na kubeba abiria kupitia kiasi kumetajwa kuwa sababu za ajali za barabarani kuongezeka. Maafisa wa usalama pia wamekuwa wakiruhusu magari mabovu kuhudumu na kuweka maisha ya abiria na watumiaji wa barabara kwenye hatari.

Ripoti kadhaa kuhusu vyanzo vya ajali zimethibitisha kuwa nyingi husababishwa na makosa ya binadamu. Ingawa ajali haina kinga, ni huzuni kubwa kwa mzazi ambaye amekuwa akihakikisha mtoto wake amejikinga asiambukizwe virusi vya corona kufahamishwa ameangamia au kujeruhiwa kwenye ajali ya barabarani ambayo inaweza kuepukwa.

Ni makosa na aibu kubwa pia kwa dereva kujikinga asiambukizwe corona na kisha kuangamia kwa sababu ya kuendesha gari akiwa mlevi au kiholela barabarani. Inasikitisha kuwa licha ya juhudi kufanywa na wadau ili kupunguza ajali za barabarani, baadhi ya madereva na baadhi ya maafisa wa usalama wanachangia kuongezeka kwa maafa haya yanayosababisha vifo vya zaidi ya watu 3000 kila mwaka.

Hivyo basi, kila anayetumia barabara ni aliyejukumiwa kutekeleza sheria za barabarani anafaa kufanya kazi yake.

Muhimu kabisa ni kwa kila dereva awe wa gari la kibinafsi, matatu au bodaboda kuthamini maisha yake. Akifanya hivi, atathamini maisha ya abiria na barabara zetu zitakuwa salama.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Mapenzi mtandaoni…raha!

JAMVI: Mvutano ODM wazidisha ubutu kwa makali ya Raila