Makala

TAHARIRI: Polisi mpakani wachunguzwe

January 21st, 2019 2 min read

NA MHARIRI

TANGU shambulizi la kigaidi litokee katika jiji la Nairobi, kumekuwa na mjadala wa kila aina kuhusu chanzo chake.

Jambo moja ambalo sote twapaswa kuliangazia kwa sasa ni jinsi ambavyo wanamgambo wa kundi la Al-Shabab au makundi mengine ya kigaii=di wanavyoweza kupenyeza ndani ya nchi yetu na kutekeleza mashambulizi.

Tatiza la kwanza ni ufisadi miongoni mwa maafisa wa usalama mpakani. Tangu Kenya ilipowatuma wanajeshi (KDF) nchini Somalia, imekuwa pia ikijenga ukuta wa kuziba eneo lake pana la mpaka.

Ni wazi kwamba magaidi wanaweza kuingia nchini kutoka Somalia au vijana wetu kuingia Somalia kufunzwa ugaidi kupitia mpakani. Je, maafisa wa polisi na wale wa uhamiaji wanaokaa mpakani huwa wako wapi?

Ina maana kuwa lazima huwa kuna ushirikiano kati ya maafisa hao na magaidi. Kama si hivyo, basi huwa maafisa wetu wa usalama wako wapi watu hawa wanapoingia au kutoka Kenya?

Pia kuna maswali kuhusu kujitolea kwa serikali kukabiliana na kuenea kwa itikadi kali miongoni mwa vijana wetu. Hali ilivyo sasa hivi, ni kuwa idadi kubwa ya magaidi ni vijana wetu wa humu nchini. Vijana hawa huenda wanasukumwa na vishawishi vinavyoweza kuzuiwa kupitia mipango thabiti.

Kuna wito kutoka kwa wadau mbalimbali kuwa maafisa wanaohusika katika mpango mzima wa kukabiliana na ugaidi wapigwe msasa.

Kwa mfano Kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudadadi anapendeleza serikali iwachukulie hatua wakuu wa usalama na maafisa wa serikali wanaopokea hongo na kuwaruhusu magaidi kuingia nchini.

Pendekezo la Bw Mudavadi ambaye mwanawe alinusurika kwenye shambulizi katika hoteli ya Dusit D2 ;afaa kuzingatiwa, hasa na Tume ya Huduma za Polisi (NPS). Mwenyekiti Johnson Kavuludi anapaswa kuwaongoza makamishna wenzake wa tume hiyo kufanya uchunguzi wa kina na kuwatambua maafisa ambao hujihusisha na ufisadi.

Aidhaserikali inafaa kuvumbua njia mpya ya kupigana na ugaidi ikizingatiwa kwamba magaidi sasa wanaishi miongoni mwa Wakenya na si Somalia pekee jinsi ilivyodhaniwa.

Vyombo vya usalama vyapaswa kutia mizani hali ya usalama nchini na kuziba mianya inayorahisisha uingizaji wa silaha hatari na magaidi nchini.