TAHARIRI: Polisi waheshimu amri za mahakama

TAHARIRI: Polisi waheshimu amri za mahakama

Na MHARIRI

Hatua ya Serikali kuendelea kumzuilia wakili na mwanasiasa Miguna Miguna katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta, (JKIA) Nairobi ni dhuluma na ukiukaji wa haki msingi za wakili huyo.

Kenya ni nchi inayoongozwa na utawala wa kisheria na inayokumbatia mfumo wa haki ambapo sheria ndio msema kweli. Yamkini, sheria inazingatiwa na kutekelezwa dhidi ya wachache.

Ni kwa nini wakili huyo anaendelea kuzuiliwa licha ya Mahakama Kuu kuamuru aachiliwe na kufikishwa mbele yake mara moja? Ni taswira gani inayojitokeza machoni pa raia wa kawaida maafisa wa polisi wanapokaidi amri za korti kiholela?

Kuna ukweli kwamba, wakili huyo huenda alivunja sheria kwa kuchelea kudai uraia wa Kenya baada ya kujisajili kama raia wa Canada. Lakini kama taifa linaloongozwa na Katiba, uhalali wa uraia wake unaweza tu kuamuliwa na mahakama.

Inasikitisha hata zaidi, maafisa wa polisi wanapojinata mbele ya waandishi habari wakidai wao ndio Serikali na kupuuza maagizo ya majaji na mahakimu.

Je, iwapo raia wangefuata mkondo wa polisi hao kudhalilisha amri za korti, nchi itaongozwa kivipi? Mfumo mzima wa sheria utasambaratika na matunda yake ni vurumai na maafa.

Idara ya polisi imejizolea sifa mbaya katika siku za hivi majuzi kutokana na namna inavyokandamiza haki msingi za raia, huku baadhi ya maafisa wakishirikiana na wahalifu kutenda maovu ya kijamii.

Wengine, hasa wale wa idara ya trafiki, wanasifika kwa kupokea hongo bila kujali wala kuogopa kushtakiwa. Sokomoko zilizotokea katika uwanja wa ndege Jumanne zinachafulia sifa idara hii ambayo kwa kweli inahusishwa na kila aina ya uozo nchini.

Tunahimiza Inspekta Jenerali Joseph Boinett kuhakikisha maafisa wake wanazingatia sheria wanapotekeleza wajibu wao. Kuvunja sheria na kukaidi amri za korti ndio mwanzo wa mwisho wa utawala wa kisheria kama tunavyoufahamu sasa.

Ni matumaini yetu kwamba, Mwanasheria Mkuu mpya Paul Kihara ambaye ni jaji mstaafu, atatoa ushauri mwafaka kwa wahusika wakuu kwenye vuta nivute inayoendelea katika JKIA ili sheria izingatiwe kwa dhati.

Kama nchi, hatuwezi kuwa na sampuli mbili za sheria; za kina yakhe na zile za mabwanyenye na wale walio na ushawishi katika jamii. Matokeo ya mpangilio kama huo ni vita na uhasama tele, na hatungependa taifa letu lichukue huo mwelekeo.

You can share this post!

Mhubiri ajuta kujenga kwenye ardhi ya umma

Wailaumu serikali ya kaunti kukosa kuwanasua kutokana na...

adminleo