Makala

TAHARIRI: Polisi wasitumie agizo kula hongo

November 6th, 2020 2 min read

KITENGO CHA UHARIRI

TANGAZO la Inspekta Jenerali wa Polisi, Hilary Mutyambai kwamba mtu yeyote atakayepatikana akikiuka kanuni za kupambana na janga la corona atatozwa faini ya Sh20,000 papo hapo limeibua wasiwasi kwa wananchi.

Kwa mtazamo wa wengi, hatua hiyo itatoa mwanya kwa polisi kuhangaisha wananchi bila sababu mwafaka

Tunaelewa kwamba huenda Bw Mutyambai alinuia kuhakikisha kuwa kila raia anafuata masharti ya kuepusha ueneaji maambukizi ya virusi vya corona kikamilifu.

Hata hivyo, ni lazima serikali ijihadhari kuhusu hatua zake isije ikafanya kuwe na madhara zaidi kwa umma.

Jinsi ilivyo kwa sasa, tayari kumekuwepo ripoti nyingi kuhusu polisi walaji hongo wanapopata mtu hana barakoa.

Tunasisitiza kuwa, ni muhimu kila mmoja avae barakoa wakati anapokuwa katika sehemu za umma.

Hata hivyo, hatua yoyote inayotoa mwanya ambao unaweza kutumiwa vibaya na polisi ni lazima ikemewe.

Wakati janga la corona lilipoingia nchini, kuna baadhi ya polisi wema ambao walijitwika jukumu la kuhakikisha mtu yeyote anayepatikana bila barakoa ananunua na kuvaa papo hapo.

Lakini kuna wale maafisa waovu ambao walitumia nafasi hiyo kujikusanyia mlungula ili kujitajirisha kibinafsi.

Itakuwa vyema kama idara ya polisi na serikali kwa jumla itawazia mbinu nyingine za kufanya wananchi warekebishe tabia zao ili kujilinda maisha yao, badala ya kufuata mbinu za adhabu kali ambazo tayari zimeonekana hazifui dafu kikamilifu.

Ikiwa idara ya polisi inadhani wananchi watundu watashtuka wakisikia kiwango cha faini watakachotozwa pale wanapopatikana wakikiuka sheria, itakuwa inajipotosha.

Kufikia sasa raia hao wameona mengi lakini bado baadhi yao hawafuati sheria. Hii ni ishara tosha kuwa mbinu za adhabu hazitoshi.

Kando na haya, hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuunda kikosi kipya cha polisi kitakachohakikisha wananchi wanatekeleza kanuni za kupambana na janga la corona, pia limepokewa kwa hisia tofauti.

Serikali itahitajika itafute jinsi itakavyowashawishi raia kwamba kikosi hicho hakitatumiwa kudhulumu haki zao za kimsingi.

Hofu imesababishwa na matukio ambayo yalishuhudiwa wakati janga la corona lilipothibitishwa nchini.