Makala

TAHARIRI: Pufya itatuharibia sifa yetu kimataifa

January 18th, 2020 2 min read

Na MHARIRI

KATIKA siku za hivi karibuni, ripoti zimezidi kutolewa kuhusu kukithiri kwa matumizi ya dawa za kusisimua misuli miongoni mwa wanariadha wa Kenya.

Ripoti ya majuzi zaidi inasema kuwa yuko mwanariadha wa Kenya aliyetoroka kambini, pale wapimaji wa matumizi ya dawa hizo kutoka shirika la kimataifa la kukabiliana na dawa hizo (WADA) walipotua katika eneo wanalofanyia mazoezi wanariadha wa Kenya eneo la Nandi.

Siku chache zilizopita, Geoffrey Kamworor ambaye hukimbia marathon alisemekana kuwatoroka wapimaji wa pufya waliofika kambini mwa Kenya kuchukua sampuli za kupima kwa dhamira ya kubaini wanaotumia pufya kujiongezea nguvu za kung’ara mashindanoni.

Matukio hayo na mengineyo ambapo wakimbiaji wetu wamepatikana kutumia dawa hizo na hivyo basi kupigwa marufuku yanazidi kuharibia taifa hili sifa kama nchi yenye wakimbiaji hodari kote duniani. Ukweli wa mambo ni kwamba Kenya inao wakimbiaji maarufu wasiotumia dawa hizo. Kwa hivyo inawezekana nchi hii kuendelea kuvuma hata bila matumizi ya pufya.

Sharti shirika la kitaifa linalopambana na matumizi ya pufya miongoni mwa wakimbiaji wetu (ADAK) likaze kamba kwa dhamira ya kutokomeza visa hivi vya kukatisha tamaa.

Nao mameneja na makocha wanaowasimamia wanariadha wanaopatikana wakitumia dawa hizi sharti waadhibiwe maadamu pana uwezekano wanawashawishi wanariadha hao kutumia dawa hizo ili washinde mbio na hivyo kuwaletea wanariadha hao pamoja na mameneja na makocha wao hao pesa na sifa.

Mchango au sauti ya serikali itakuwa muhimu katika kuimarisha vita dhidi ya dawa hizi, hasa wakati huu ambapo taifa linajiandaa kwa Michezo ya Olimpiki itakayofanyika jijini Tokyo, Japan kuanzia Julai 24 hadi Agosti 9.

Kutochukua hatua kali dhidi ya uovu huo ni kama chachandu kujipalia makaa mwenyewe kwani pana uwezekano mkubwa taifa hili likapigwa marufuku na shirikisho la riadha ulimwenguni (IAAF) kama ilivyofanyika kwa Urusi punde baada ya Olimpiki za Rio, Brazil, 2016.

Kwa sasa hakuna mwanariadha yeyote wa taifa hilo kubwa na maarufu anayeruhusiwa kushiriki mashindano ya IAAF baada ya marufuku hiyo kutolewa.

Wahenga walisema tahadhari kabla ya hatari; tamathali hiyo yafaa iwe kiongozi chetu wakati huu panapojitokeza dalili nyingi kuwa hatari inaweza kutufika.