Makala

TAHARIRI: Raia wachague viongozi wanaofaa

April 3rd, 2019 2 min read

NA MHARIRI

UCHAGUZI mdogo katika maeneo ya Ugenya na Embakasi Kusini utafanyika kesho ambapo wapiga kura maeneo hayo wanatarajiwa kuwachagua viongozi wao.

Maeneo haya yanafanya uchaguzi wakati ambapo mtazamo wa kisiasa nchini umebadilika hasa tangu muafaka ulipofanyika kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga. Msingi mkuu wa kusalimiana kwao, ulikuwa kutuliza joto la kisiasa nchini.

Hata hivyo, maswali mengi yameulizwa kulingana na jinsi mambo yanavyoendelea nchini,hasa iwapo upinzani ungali upo nchini.

Waliotajwa kama wapinzani wameshuhudiwa mara kadha katika hafla za serikali, tukio la hivi punde likiwa uzinduzi wa Huduma Namba uliofanyika kote nchini na kuwahusisha viongozi wanaoegemea kwa upinzani kama Bw Odinga, Kalonzo Musyoka wa Wiper na hata Musalia Mudavadi wa ANC.

Kwa hivyo, Wakenya katika maeneo haya yanayoandaa uchaguzi, wanafaa kutilia maanani kile wanachotarajia kutoka kwa viongozi wanaowachagua na sio kufungwa macho kwa misingi ya vyama au wanachoshawishiwa nacho kutoka kwa wagombeaji.

Uchaguzi huu unafaa kuwapatia matamanio ya mioyo yao kama kupelekewa maendeleo ya kuinua maisha na kuyajenga maeneo yao.

Lazima pia wajitahidi kuzuia kuchochewa kwa sababu ya viongozi kwa kuwa yaliyofanyika kati ya Rais na Bw Odinga ni dhihirisho kuwa siasa hazina maadui wala marafiki wa kudumu. Lazima watu watekeleze jukumu hilo la kupiga kura bila vurugu zozote.

Chaguzi hizi ndogo za Ugenya na Embakasi zinapofanyika pia zinafaa kuangaziwa na Wakenya wengine kuweza kutafakari ikiwa kuna mafunzo yoyote ambayo wamejifunza.

Hii ni kwa sababu mara nyingi watu hupigia watu fulani kura na baadaye kugeuka kulalamika kuwa hawatimizi walichotarajia.

Katika eneo la Embakasi, wawaniaji wawili ni watu ambao wote wamepata fursa ya kuwakilisha eneo hilo, na wapiga kura wa eneo hilo wana nafasi bora zaidi ya kufanya uamuzi wa busara bila kushinikizwa na vyama.

Ni wakati ambapo taifa hili linafaa kuanza kuzingatia aina ya watu inayowaweka mamlakani ili kuzuia lawama za kila wakati ambapo wapigakura wamehisi kuvunjika moyo wanapopata kuwa matarajio yao hayatimizwi. Lazima wajifunze kuweka vigezo wanavyotaka wenyewe kwa kiongozi.