TAHARIRI: Raia wasikubali kuyumbishwa

TAHARIRI: Raia wasikubali kuyumbishwa

KITENGO CHA UHARIRI

JUMANNE ilikuwa siku ya historia ambapo kaunti zaidi si chini ya 26 zilifanya uamuzi na kuungana na zingine 12 kuidhinisha Mswada wa marekebisho ya Katiba (BBI).

Hata kaunti zilizotarajiwa kuchukua mwelekeo wa Baringo kukataa Mswada huo, zilishangaza Wakenya kwa kuupitisha kwa kauli moja.

Madiwani katika kaunti kama Bomet, Narok, Nakuru na Isiolo walitarajiwa kuukataa ikizingatiwa wanasiasa wakuu wa maeneo hayo wamekuwa wandani sugu wa Naibu Rais William Ruto.

Ingawa Dkt Ruto hajatangaza hadharani kupinga mswada wenyewe, amenukuliwa zaidi ya mara moja akisema mageuzi hayo si muhimu kwa vile yanalenga kuwaundia nyadhifa watu wachache.

Kwa hivyo, maseneta Ledama Ole Kina (Narok) na Susan Kihika (Nakuru) walitarajiwa kwamba wangeweza kushawishi madiwani kwenye kaunti zao kukataa mswada. Bomet kwa kuwa ni mojawapo ya ngome kuu za Dkt Ruto ilitarajiwa ingepiga kura sawa na Baringo.

Ni juzi tu ambapo Dkt Ruto alilakiwa na umati mkubwa Isiolo. Madiwani wa huko pia waliamua kwamba historia ya marekebisho ya Katiba itakapoandikwa, hawangependa kusahaulika.

Zimesalia kaunti nane ambazo hazijatoa kauli; japo hitaji la kikatiba kwamba Mswada upitishwe na mabunge angalau 24, limetimizwa.

Sasa Mswada utaenda kwa Bunge la Kitaifa na la Seneti kabla ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuunda swali na kuliwasilisha kwa wananchi watoe uamuzi wa mwisho katika kura ya maamuzi.

Mwananchi ndiye mwenye kauli katika suala hili. Wanasiasa wataanza kujipeleka mashinani kuhubiri kila aina ya propaganda. Wapo watakaoukosoa mswada na wengine kuupigia debe, bila ya kuwaeleza wananchi manufaa au mabaya yake.

Muda uliobaki hadi wakati wa kura ya maamuzi unatosha kabisa kwa raia kuchukua nakala za BBI na kuanza kujisomea. Wale ambao hawajui kusoma watafute usaidizi kutoka kwa watoto wao au walimu walio karibu nao.

Uamuzi utakaotolewa kuhusu Mswada huu ni muhimu sana kwa nchi, kwa kuwa, miongoni mwa mengine, utaamua jinsi wananchi wanataka kutawaliwa.

Kwa mfano, japokuwa Waziri Mkuu na wasaidizi wake wawili watakuwa wabunge, kunapendekezwa kuwe na wabunge wa ziada 117. Kwa upande mwingine, pesa za kaunti zitaongezwa ili wananchi wanufaike mashinani. Uamuzi usifanywe kwa kuzingatia maneno ya kusikia kutoka kwa wanasiasa.

You can share this post!

BI TAIFA FEBRUARI 24, 2021

Kwani kuliendaje?