Maoni

TAHARIRI: Rais ahakikishe anatimiza ahadi zake kwa vijana

June 28th, 2024 2 min read

BAADA ya Rais William Ruto kufanya uamuzi wa kutotia saini mswada tata wa fedha, ametoa ahadi nyingi kuhusiana na masuala ya fedha na jinsi ambavyo anapanga kushirikiana na vijana.

Hatua hiyo inastahili hata ingawaje ilichukuliwa kuchelewa hasa baada ya taifa kupoteza maisha ya vijana wenye nguvu na ambao huenda wangelifaa taifa hili kwa njia mbalimbali.

Hatua yake inadhihirisha kuwa kilio cha vijana ambao wamekuwa wakiandamana kilikuwa na msingi na kwamba ipo haja ya matakwa yao na ya wananchi wengine kwa jumla kuangaliwa ili kuweza kubaini jinsi ya kutatua mambo kabla hayajafikia kiwango kilichoshuhudiwa Jumanne hasa katika majengo ya Bunge.

Hata hivyo, Rais na wengine wakiendelea kutafuta suluhu, ni muhimu kutafakari kwa kina chanzo cha hasira hii. Bila shaka, mswada huu si sababu pekee.

Ni muhimu kujaribu kuelewa sababu ya watu wengine kuamua kuwaunga mkono kama kuwapatia waandamanaji maji ya kunywa na chakula.

Mbona wachukue hatua hiyo? Si kweli kwamba waliwaonea imani tu.

Ni jambo muhimu kutafakari kwani mojawapo ya sababu zao ni kwamba hata nao wana malalamishi yao, lakini huenda hawajapata nguvu za kujitokeza hadharani kusema yao ya moyoni, na kuwaona vijana wao wakichukua hatua ambayo labda wamekuwa wakiitamani, kuliwapatia matumaini mapya.

Ni muhimu pia kwa viongozi wa taifa hili kutafakari kwa kina kuhusu matamshi yao. Yapo matamshi ambayo badala ya kujenga, yanavunja na kukeketa maini.

Lakini zaidi ni ukabila. Kuona jinsi wanavyoshindania nyadhifa kwa sababu ya ukabila ilhali taifa hili lina makabila mengi.

Mwelekeo huu uliochukuliwa na vijana wa kutaka kuona taifa likiwa na umoja wa kweli, linastahili kuzingatiwa kwa kuwa wameeleza kuwa wao hawatambui suala la ukabila, muhimu kwao ni kuona nchi ikisonga mbele na kuwapatia fursa za kujikuza.

Kadhalika, lipo suala ambalo lazima liangaliwe kwa makini. Idadi kubwa ya vijana nchini.

Ni vipi ambavyo taifa litasaidia kubuni ajira pamoja na kuweka mazingira bora na faafu kwao kujibunia ajira na kutafuta namna za kujikimu.

Hii ni kwa sababu, bila kufanya hivyo, wataendelea kudai nafasi yao mezani.

Kwa sasa, wengi wanasubiri waliopo mamlakani kutoa mwelekeo na kusaidia kuimarisha kizazi hiki ambacho kikijumuishwa mezani, bila shaka hakitakosa mawili matatu ya kusaidia kuimarisha mustakabali wao katika taifa na ulimwengu huu.