Makala

TAHARIRI: Rais si wa Mlima Kenya pekee

January 9th, 2019 2 min read

NA MHARIRI

MJADALA unaoendelea sasa hivi kote nchini kuhusiana na matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta, wafaa uangaliwe kwa busara na ukomavu.

Rais Kenyatta alipowaita watu fulani “Washenzi” kwa kumkosoa anapotembea kila pembe ya nchi kuzindua miradi, alikuwa na maana kuwa msimamo wa aina hiyo ni wa watu wasiokuwa na ustaarabu.

Yaani kuna viongozi waliochaguliwa na wananchi katika wadi, eneo bunge au kaunti ili wawe karibu na wananchi. Isitoshe, baadhi yao wako na hazina maalum za kuwawezesha kutekeleza miradi mbalimbali. Lakini kwa kukosa maarifa ya uongozi, huwa wanamsubiri kiongozi wa nchi awapelekee maendeleo.

Katiba yetu tuliyoipitisha mwaka 2010 inaeleza wazi kuwa Rais ni ishara ya Utaifa na kwa hivyo, punde tu anapoapishwa, anakuwa si mali ya eneo alikozaliwa.

Japokuwa Rais Kenyatta alizaliwa Gatundu, Kiambu yeye si Rais wa watu wa eneo la Mlima Kenya pekee. Ana wajibu wa kuzunguka nchi yote, na kukagua miradi na maendeleo yaliyotekelezwa.

Wabunge Moses Kuria na Kimani Ngunjiri kabla hawajamshutumu rais kuwa amepuuza jamii ya watu wa Mlima Kenya, wanapaswa waeleze wananchi wametumia vipi pesa za Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneo Bunge (NGCDF).

Mwaka wa kifedha wa 2018/19 eneo bunge la Gatundu Kusini lilipewa Sh 109,040,875.52. Je, hizi si pesa za kufanya japo mradi mmoja mkubwa?

Isitoshe, Kaunti ya Kiambu chini ya Gavana Ferdinand Waititu ‘Baba Yao’ ilipewa Sh9.35 bilioni. Mgao huu unaifanya Kiambu kuwa kaunti ya saba kwa kupata pesa nyingi baada ya Nairobi, Kilifi, Turkana, Kakamega, Mandera na Nakuru. Vigezo vilivyotumika mbali na idadi ya watu, ni ukubwa wa eneo na umasikini.

Kwa Bw Kuria kuendeleza majibizano na rais hadharani, ni kuonyesha hajatambua Katiba, ambayo ndiyo dira ya kuongoza wabunge wanapotunga sheria.

Maendeleo yote mashinani ni jukumu la serikali za kaunti chini ya magavana. Iwapo kuna mradi mkubwa wa serikali ya kitaifa hapo Rais anaweza kuuzindua.

Kwa hivyo, wanasiasa waache kudanganya wananchi kuwa maendeleo hayapatikani iwapo rais hajawatembelea.