Makala

TAHARIRI: Sasa matumaini yote ni kwa BBI

October 17th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

KUKATALIWA kwa Mswada wa ‘Punguza Mizigo’ na kaunti za Migori, Marsabit, Kitui, Mombasa na Nyandarua jana, kulifikisha idadi ya kaunti hizo kuwa 28.

Moja kwa moja, hata bila ya kusubiri kujua kama zipo kaunti zinazoukubali au la, mswada huo umeangushwa. Katiba inasema kwamba Sheria inayopanga kufanya mabadiliko yoyote katika Katiba yafaa iungwe mkono na angalau kaunti 24 kati ya 47.

Katika kukataa mswada huo uliowasilishwa na chama cha Thirdway Alliance cha Dkt Ekuru Aukot, wawakilishi wadi katika mabunge ya kaunti walidai kuwa wananchi hawakushirikishwa na wala mapendekezo yake hayatekelezeki.

Kile ambacho MCAs hao hawataki kuwaambia Wakenya ni kuwa walichukua uamuzi huo baada ya kuingiza siasa katika suala hilolililokuwa la kisheria. Mswada wa Punguza Mizigo miongoni mwa mambo muhimu ni kupunguza mishahara ya watumishi wa umma. Pia, ulilenga kumaliza ufisadi kwa kulazimu idara ya Mahakama iwe ikimaliza kesi za ufisadi katika siku 30.

Punguza Mizigo ilipendekeza kuwe na vipengee vya ziada katika Kifungu cha 79 cha Katiba ili viseme, “Kesi za Ufisadi au wizi wa mali ya umma zitasikizwa na kuamuliwa katika kipindi cha siku 30 na washukiwa watakata rufaa katika kipindi cha siku 21 baada ya uamuzi.

Kwamba, yeyote atakayeshtakiwa na apatikane na hatia ya ufisadi au wizi wa mali ya umma, afungwe jela maisha.

Na kwamba, bila kuzingatia kifungu cha 133 cha Katiba, Rais hatakuwa na mamlaka ya kumsamehe mfungwa anayetumikia adhabu ya kuwa mfisadi au kuiba mali ya umma.

Kwa kukata miguu ufisadi, Kenya ingeweza kuwa na pesa nyingi zinazoweza kutumika kutekeleza miradi mingi ya maendeleo. Ni pesa hizo ambazo zingeongezwa kutoka asilimia 15 ya bajeti inayopelekwa kwa Kaunti na kufikia asilimia 35.

Punguza Mizigo ilikuwa imependekeza kuwa pesa hizo zitumike katika ngazi ya Wadi, ambako ndiko kuliko na wapigakura. Lakini kwa kuwa wawakilishi wadi wanaegemea mirengo ya ‘handisheki’ na ‘Tangatanga’ waliamua kukataa mageuzi hayo muhimu kwa kisingizio kuwa sheria ingepunguza idadi ya wabunge na kuwanyima wanawake nafasi za uongozi.

Kukataliwa kwa Punguza Mizigo kuna maana kuwa, matumaini yote sasa ni kwa ripoti ya BBI, iwaokoe wananchi.