Makala

TAHARIRI: Sekta ya afya yahitaji mageuzi

November 16th, 2020 2 min read

KITENGO CHA UHARIRI

MASAIBU yaliyomkumba mtangazaji wa zamani wa redio, Bw Leonard Mambo Mbotela, kuhusu malipo ya matibabu hivi majuzi yaliibua upya mjadala kuhusu hali ya afya nchini.

Bw Mbotela alikuwa amezuiwa katika hospitali ya Nairobi kwa kushindwa kugharimia malipo ya matibabu yaliyofika zaidi ya Sh1 milioni.

Tukio hilo limekuwa kama kawaida kwa wananchi wengi, ambao hushindwa pa kugeukia wanapohitajika kulipa pesa nyingi mno za matibabu, iwe ni katika hospitali za umma au za kibinafsi.

Wakati Rais Uhuru Kenyatta alipohutubia taifa wiki iliyopita, alisema utawala wake ulilenga kuondolea wananchi gharama kubwa ya matibabu kupitia mpango wa afya bora kwa wote, almaarufu kama UHC.

Wananchi wengi walitarajia kuwa mpango huo ambao ulifanyiwa majaribio katika kaunti za Kisumu, Machakos, Nyeri na Isiolo ungeendelezwa punde baada ya kipindi cha majaribio kukamilika lakini sasa ni bayana kuwa hali sivyo.

Ijapokuwa sekta ya afya iko chini ya serikali za kaunti kikatiba, kama kuna ajenda moja kati ya nne ambazo Rais Kenyatta angetuza nayo Wakenya kabla aondoke mamlakani mwaka wa 2022, ingekuwa ni kufanikisha mabadiliko katika sekta hiyo hasa kuhusu gharama ya matibabu.

Sekta hiyo inakumbwa na changamoto tele katika hospitali za umma ambazo zinategemewa na idadi kubwa ya wananchi.

Miundomsingi duni, uhaba wa vifaa na dawa, uhaba wa wahudumu wa afya imekuwa desturi katika hospitali hizo kote nchini.

Isitoshe, licha ya kuwa zinategemewa na wananchi wengi wa mapato ya chini, gharama ya matibabu kwa magonjwa kadhaa huwa ni ya juu mno.

Itakuwa vyema kama wadau wote katika sekta ya afya watakubaliana kuhusu njia bora zaidi ya kuiboresha kwa manufaa ya wananchi.

Janga la corona lilifichua uozo mwingi katika baadhi ya kaunti zetu ambapo ilibainika huduma za afya kwa umma ni duni mno.

Magavana wanapopigania mamlaka zaidi kusimamia afya, wajihoji kama kweli serikali zote za kaunti zina uwezo kusimamia jukumu hilo muhimu. Vile vile, serikali kuu ifanye utathmini wa mipango yake inapoingilia jukumu hilo.