Makala

TAHARIRI: Sekta ya michezo inahitaji suluhu

October 5th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

SEKTA ya michezo nchini inapitia changamoto tele zinazohitaji kutafutiwa suluhu upesi.

Kauli hii inachochewa na ripoti kuwa kocha wa timu ya Kenya ya voliboli, Paul Bitok hajalipwa mshahara maadamu shirikisho la mchezo huo nchini (KVF) halina pesa za kutosha.

Huenda tatizo hilo ndilo lililofanya Kenya kutandikwa katika takribani mechi zote wakati wa shindano la dunia la mchezo huo. Katika mechi zake, Kenya ilifanikiwa kulaza Cameroon pekee huku ikilemewa katika mechi tano dhidi ya mataifa mbalimbali ya mabara ya ulimwengu.

Katika mashindano kama haya, wachezaji pamoja na benchi la ufundi huhitajika kuwa na motisha ndipo wawe na nafasi ya kufanya vyema; mazoezi mazuri pekee hayasaidii.

Kutokana na ugumu huo, KVF imeomba serikali kupitia kwa Wizara ya Michezo kuanza kulisaidia kulipa kocha jinsi ilivyo kwa mchezo wa soka ambapo serikali ndiyo hulipa kocha wa timu ya taifa.

Tatizo hili limekuwa sugu zaidi si kwa mchezo wa kimia pekee bali hata katika fani nyinginezo za michezo; si soka, si raga, si riadha, si mpira wa vikapu, almuradi kila sekta ya michezo imejaa changamoto.

Hii ndiyo maana pana haja ya serikali kubuni mikakati madhubuti ya kuokoa sekta ya michezo nchini.

Mojawapo ya mambo yanayofaa kuangaliwa kwa undani zaidi ni mgao ambao serikali hutengea sekta hii katika bajeti yake kila mwaka. Ina maana kuwa mgao huo huwa mdogo zaidi kiasi cha kutatiza maendeleo ya michezo nchini kwa njia nzuri. Hivyo basi, ni vyema kwa serikali kuzingatia kuongeza pesa inazotengea idara hiyo.

Ifahamike kuwa sekta ya michezo ni mojawapo ya vitengo vinavyoweza kusaidia serikali kupunguza ukosefu wa nafasi za ajira hasa miongoni mwa vijana.

Aidha pana haja pia ya mashirikisho mbalimbali ya michezo pamoja na wadau katika sekta hiyo kuanza kubuni sera zitakazowezesha timu hasa za kitaifa kuwa na pesa za kutosha kuendesha shughuli bila kutegemea serikali pekee.

Sharti sera zitakazovutia mashirika hisani na watu binafsi kufadhili michezo. Aghalabu kinachosababisha wafadhili kutoroka ni sera mbovu na uongozi duni miongoni mwa mashirikisho yetu ya michezo.

Itakuwa bora, vilevile kuyaiga mataifa yaliyopiga hatua ya maana katika michezo kama mojawapo ya dawa ya kumaliza matatizo katika mashirikisho yetu.