TAHARIRI: Sekta ya uchukuzi ikombolewe sasa

KITENGO CHA UHARIRI

HATUA ya baadhi ya makampuni ya mabasi kusitisha shughuli zao za uchukuzi wa abiria inafaa kuzindua serikali kutoka usingizini kuhusu hali mbaya ya mandhari ya kufanyia biashara humu nchini.

Kampuni za Modern Coast na Mombasa Raha hivi majuzi zilithibitisha kusitisha safari za abiria kwa sababu ya hasara ambazo biashara ya uchukuzi imekuwa ikikumbana nazo hasa maeneo ya Pwani.

Matatizo yalianza punde baada ya uzinduzi wa treni ya SGR, ambapo abiria wengi waliokuwa wakitegemea mabasi kusafiri hadi Nairobi walipotambua inachukua muda mfupi kusafiri kwa reli.

Ijapokuwa makampuni ya mabasi yalipitia changamoto tele, wamiliki walivumilia kwani kulikuwa bado angalau kuna biashara kusafirisha abiria hadi maeneo mengine ya nchi.

Pigo kubwa lilitokea baada ya kanuni kali kupitishwa kuhusu mbinu za kuzuia ueneaji wa virusi vya corona kuanzia mwaka uliopita.

Kanuni zinazolenga magari ya uchukuzi wa umma zimedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa ambapo magari hayo huhitajika kubeba takriban nusu ya idadi ya kawaida ya abiria.

Kumekuwa na malalamishi miongoni mwa baadhi ya wawekezaji katika sekta ya uchukuzi wa umma, wakidai kuna ubaguzi katika utekelezaji wa kanuni hizo.

Hii ni kutokana na kuwa, treni na ndege zinaruhusiwa kubeba idadi kamili ya wasafiri ilhali mabasi na matatu zimekatazwa kufanya hivyo.

Tetesi ni kuwa, wananchi wengi hawaelewi kwa nini wanakubaliwa kutagusana na wenzao wanapoabiri ndege au treni kisha wanapoenda kuabiri mabasi au matatu wanaambiwa ni sharti wakae mbali na wenzao.

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya afya wamejaribu kueleza kuwa ni rahisi kuhakikisha kanuni za kuepusha ueneaji wa virusi vya corona kutekelezwa kikamilifu katika ndege au treni kuliko katika vyombo vingine vya uchukuzi wa umma.

Kanuni zinazotajwa ni kama vile uoshaji mkono mara kwa mara, kutumia vieuzi kusafisha mikono na hitaji la abiria wote kuvaa barakoa wakati wote wakiwa ndani ya ndege au treni.

Hata hivyo, ni sharti serikali itafute mbinu zitakazookoa sekta ya uchukuzi wa umma isiporomoke sawa na sekta nyingine nyingi ambazo zinaendelea kuathirika kutokana na makali ya janga la corona.

Wanaoathirika si wafanyabiashara moja kwa moja bali pia wawekezaji wengine wanaotegemea safari za abiria kwa biashara zao.

Habari zinazohusiana na hii