Makala

TAHARIRI: Semi za Trump tishio kwa haki na usawa

July 20th, 2019 2 min read

Na MHARIRI

ILIKUWA wiki iliyojaa malumbano tele nchini Amerika, taifa lililo na nguvu zaidi ulimwenguni na linaloangaliwa kwa karibu kutokana sifa za usawa, haki na demokrasia iliyokuja kulitambulisha kwa zaidi ya miaka 200 tangu libuniwe.

Kwa jambo lililoanza kama ubishani wa ‘kawaida’ kati ya vyama hasimu vya Republican na Democrats, liligeuka sura kwa haraka na kuwa majibizano ya kushtua baina ya Wabunge wanne wa kike walio na asili ya Kisomali, Kilatina, Kiafrika na Kipalestine na Rais Donald Trump.

Kundi la wabunge hao; Alexandria Ocasio Cortez (Asili ya Puerto Rico), Ilhan Omar (asili ya Kisomali) Aynna Pressley (Mwamerika Mweusi) na Rashida Tlaib (Asili ya Kipalestina) wanaojiita “Progressive Democrats” ambao kimsingi wanatetea na kushinikiza mageuzi ya sera kuhusu elimu, uhamiaji na masuala ya ubaguzi wa rangi lilikuwa kwenye harakati za kushinikiza uongozi wa chama chao chenyewe, unaoshikiliwa na Spika Nancy Pelosi kukaza kamba zaidi katika mvutano wao dhidi ya Serikali ya Trump.

Lakini Rais huyo alidakia mazungumzo hayo na kuandika kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba wabunge hao wanne walio na asili ya Kiafrika “wanafaa kurudi kwa nchi zao mbovu kama hawafurahii maisha Amerika”.

Ama kwa hakika ni matamshi yaliyozua hamaki kutoka pande nyingi huku wengi wakitaja semi hizo kuwa za chuki na za kibaguzi ambazo hazifai kuhusishwa na kiongozi anayeshikilia mamlaka ya urais katika taifa hilo lililojengwa na wahamiaji.

Viongozi kama Angela Merkel ambaye taifa lake la Ujerumani lingali linapona kutokana na makovu ya uongozi wa kikatili na kibaguzi uliokuwa na Adolf Hitler alikemea matamshi hayo akitayataja kuwa ya kibaguzi na ambayo yanatishia hata maisha yenyewe na wabunge hao walio na asili ya ‘kigeni’.

Itakumbukwa kwamba semi za “warudi kwao” zimetia wengi mashakani, na wa hivi majuzi hapa nchini akiwa Mbunge wa Starehe Charles Njagua aliyezua malumbano na nchi jirani ya Tanzania.

Kwa ulimwengu wa sasa unaotawaliwa na utandawazi, hakuna aliye na haki ya kumwambia mwingine “aende alikotoka” kwa sababu demokrasia hazina budi kutoa nafasi kwa hisia tofauti na kinzani kwa sababu zaidi ya yote kila binadamu anamhitaji mwenziwe.