Makala

TAHARIRI: Sera kuhusu tuzo za taifa ziwe wazi

October 21st, 2019 2 min read

Na MHARIRI

WANANCHI wengi Jumapili walipendezwa na jinsi serikali ilivyomtuza mshikilizi wa rekodi ya mbio za marathoni duniani Eliud Kipchoge tuzo ya hadhi ya juu zaidi ya taifa kwa raia, ya Elder of the Order of the Golden Heart (EGH).

Wakati Kipchoge aliletea Kenya fahari kubwa hivi majuzi kwa kukimbia marathoni kwa chini ya saa mbili jijini Vienna, Austria, serikali ilijikuta pabaya ikilaumiwa kwa jinsi ambavyo haijawahi kumtuza chochote mwanariadha huyo ambaye amekuwa fahari ya nchi hii kwa miaka mingi.

Hii ni licha ya kuwa tumeona tuzo za kitaifa zikipeanwa kwa watu ambao, kimsingi, hawastahili kupewa tuzo hizo.

Hatua ya Jumapili huenda ilitokana kwa kiasi fulani na shinikizo lililotolewa na Wakenya kutaka serikali imwonyeshe Kipchoge taadhima ya kipekee.

Kwa msingi huu, inatakikana kuwe na sera za wazi kuhusu watu wanaofaa kupewa tuzo hizo kwani si za mtu binafsi bali ni za taifa.

Inaridhisha kusikia ripoti kwamba kuna hatua zilizowekwa ili kuhakikisha kwamba wale waliotuzwa baada ya sherehe za jana walikuwa watu waliostahili na wala hawapewi tuzo kwa msingi tu wa kuwa wandani wa wenye ushawishi serikalini.

Tungependa sera zote kuhusu tuzo hizo ziwe wazi kwa wananchi wote ili tuzo zinapotolewa, kila mmoja aweze kuweka kwenye ratili na kuona kama wanaotuzwa walifikia kiwango kilichoekwa.

Zaidi ya hayo, itakuwa bora kama wananchi watapewa nafasi ya kuchangia katika sera zinazoongoza shughuli hiyo nzima ya uteuzi wa mashujaa wa kitaifa kila mwaka.

Hii itazuia hali kama ile iliyoshuhudiwa mwaka wa 2017 ambapo wananchi walibaki wakiwa na hasira zaidi ya mshangao wakati orodha ya waliopewa tuzo za kitaifa ilipotangazwa wazi.

Orodha hiyo iliacha wengi wakishangaa wale waliokuwemo walitoa mchango upi kwa ustawi wa nchi, isipokuwa uhusiano wao wa karibu na wanasiasa wenye ushawishi serikalini na pengine, sarakasi zao mbele za umma.

Katiba ilikuwa na nia njema sana ilipoamua Sikukuu ya Kenyatta Dei ibadilishwe kuwa Mashujaa Dei, na hivyo basi inastahili siku hii isichafuliwe kwa kutoa tuzo za heshima za taifa kwa wasiostahili.