TAHARIRI: Sera mpya ya kifedha ya Ruto itaokoa raia wengi

TAHARIRI: Sera mpya ya kifedha ya Ruto itaokoa raia wengi

NA MHARIRI

RAIS William Ruto jana Alhamisi alitangaza mikakati kabambe ya kifedha inayoweza kulikwamua taifa hili kutokana na hali mbaya ya kiuchumi inayowakeketa Wakenya.

Miongoni mwa mipango hiyo inayostahili kuungwa mkono kwa dhati ni agizo la kupunguza bajeti za wizara na idara za serikali ili kuokoa takribani Sh300 bilioni ambazo kwa kawaida hutengewa matumizi yasiyokuwa ya kimsingi.

Aidha, Rais ameahidi kupunguza kiwango kinachokopwa, hasa kutoka kwa mashirika ya kimataifa, na badala yake kubuni sera mpya inayowahimiza Wakenya kuweka akiba zaidi ili wajitegemee kibinafsi na kitaifa.

Akiba hiyo, ambayo ni Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF), itaiwezesha serikali kukopa pesa humu nchini na kuwekeza kisha kuzilipa kwa riba.

Ili kuvutia Wakenya kupenda mazoea ya kujiwekea akiba, Rais Ruto alisema kuwa serikali yake itakuwa ikiongeza Sh1 kwa kila Sh2 ambazo mwananchi atakuwa akiweka kwenye NSSF.

Siku moja kabla, Dkt Ruto alionekana kuanza kutekeleza mfumo wake wa ukuzaji wa uchumi kuanzia tabaka la chini almaarufu Bottom-Up.

Hii ni baada ya kuafikiana na benki na mashirika mengine ya kifedha ikiwemo kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kulegeza masharti ya ukopaji wa pesa.

Miongoni mwa masharti hayo ni kupunguza riba, kwa mfano, inayotozwa kwa wanaokopa deni la Fuliza mbali na kujiepusha na kuorodhesha Wakenya katika CRB kiholela.

Mbali na mikakati mingine kabambe anayotarajiwa kutangaza hivi karibuni, Rais ameonyesha nia ya dhati ya kuauni uchumi wa taifa hili ambao kwa miaka mingi umekuwa na manufaa kwa mabwanyenye huku mamilioni ya raia wakisota kwenye umaskini.

Inapozingatiwa kuwa Rais mwenye alitoka katika familia maskini, basi ipo imani kubwa kwake kwamba anajua matatizo ya kimsingi ni yepi na hivyo basi atabuni suluhisho la kudumu kwa manufaa ya Wakenya wote, hasa wanaoitwa mahsla.

Vilevile, Dkt Ruto ameonyesha kuwa nia yake kuu itakuwa kuimarisha sekta ya kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa hili.

Hata hivyo, ingawa ni mapema kumtia Rais kwenye mizani hasa kuhusiana na juhudi za ufufuzi wa uchumi, ni muhimu pia kumhimiza atilie mkazo maoni ya upinzani hasa pale alipoombwa jana kukumbuka kuelezea mkakati wake wa kukabiliana na ufisadi ambao hufyonza takribani Sh700 bilioni kwa mwaka.

Letu kwa sasa ni kumuunga mkono Rais mbali na kumtakia kila la heri.

 

  • Tags

You can share this post!

Katungwa aendelea kuhangaisha mabeki soka ya wanawake India

Raga ya Impala Floodlit kurejea Oktoba baada ya miaka miwili

T L