TAHARIRI: Serikali ichunguze wanachofanya waliopewa leseni za kumiliki silaha

TAHARIRI: Serikali ichunguze wanachofanya waliopewa leseni za kumiliki silaha

NA MHARIRI

SERIKALI yafaa ichunguze waliopewa leseni za kumiliki bunduki nchini, ijulikane wanazitumia kwa kazi gani.

Kuna watu wengi ambao wanadai wana leseni za kumiliki bunduki ila baadhi japo ni halali, wamekuwa wakitumia silaha hiyo kwa njia isiyofaa au hata kuikodisha kwa wahalifu.

Mnamo Jumatano, polisi walitwaa bunduki 22 na risasi 500 katika afisi mmoja mtaani Kilimani. Polisi hao walikuwa wakitoa ulinzi kwa madalali waliokuwa wakitekeleza amri ya korti dhidi ya mmiliki wa afisi hizo Bw Wycliffe Lugwili ambaye alikuwa akidaiwa Sh4 milioni.

Swali hata hivyo, ni je bundiki hizo zilitoka wapi na zilihifadhiwa hapo kwa lengo gani? Na pengine huenda zimekuwa zikitumika kutekeleza misururu ya visa vya uhalifu jijini Nairobi na maeneo ya mengine?

Ripoti ya shirika moja mwaka huu ilionyesha kuwa Wakenya 70,000 wamepata bunduki za matumizi ya kibinafsi tangu Juni 2018. Mnamo 2020, Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i alisitisha kutolewa kwa leseni baada ya kuongoza oparesheni za kutwaa silaha haramu, ila bado bunduki nyingi zi mikononi mwa raia.

Wakati wa oparesheni hizo bunduki haramu 8,628 na risasi 370,000 ziliharibiwa, huku Dkt Matiang’i akiamuru kuwa wanaomiliki bunduki wajisajili tena. Hata hivyo, bado haijatolewa taarifa kuhusu iwapo wengi walizingatia amri hiyo na kurefusha upya matumizi ya leseni yao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 4000 wanaomiliki bunduki walitajwa kama waliojihami vikali na hatari kwa usalama baada ya kukosa kurefusha upya leseni zao.

Hata hivyo, Dkt Matiang’i anafaa kuamrisha oparesheni ifanyike upya kuhakikisha kuna usalama wa kutosha hasa wakati huu ambapo taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9. Wakati huu wanasiasa wanaposaka kura, wanaweza kuwapa vijana silaha hizo ili kutibua mikutano ya wapinzani wao.

Dkt Matiang’i anafaa kuamuru oparesheni hiyo ifanyike katika maeneo ambako wizi wa mifugo umekithiri katika kaunti za Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi na Baringo. Haipiti wiki kabla ya mauaji kuripotiwa huku jamii hizo zikiwa na silaha hizo ila haifahamikiwa wanakozitoa au kuuziwa.

Ni kutokana na uwepo wa silaha hatari mikononi mwa raia ambapo serikali inaonekana imeshindwa katika kumaliza vita dhidi ya wizi wa mifugo ambavyo vimedumu katika karibu tawala zote tangu Kenya ijinyakulie uhuru.

Usalama wa nchi kwa sasa ni jambo ambalo linafaa kupewa kipaumbele na serikali hasa wakati huu ambapo taifa linakaribia uchaguzi mkuu. Iwapo bunduki haramu zitazidi kuwa mikononi mwa raia, basi kuna kila sababu ya watu kuhofia usalama wao.

  • Tags

You can share this post!

Rais Kenyatta akataa kutia saini mswada wa kuumiza...

VALENTINE OBARA: MCAs waelezee wanayokamia kufanyia raia...

T L