TAHARIRI: Serikali idhibiti mashirika yanayopeleka Wakenya ng’ambo kusaka ajira

TAHARIRI: Serikali idhibiti mashirika yanayopeleka Wakenya ng’ambo kusaka ajira

NA MHARIRI

UKIMYA wa serikali ya kitaifa kuhusu malalamishi ya wakazi wa Uasin Gishu dhidi ya shirika moja la kusaidia Wakenya kupata ajira ughaibuni, unazua maswali tele.

Wiki hii, shirika hilo la First Choice Recruitment and Consultancy linatarajiwa kusafirisha karibu Wakenya 120 katika nchi za Poland, Qatar na Italia kusaka kazi za kufanya usafi, kuhudumu hotelini, ulinzi na utunzaji wa bustani.

Shirika hilo jana Jumapili liliandaa ibada ya maombi kabla ya kuanza safari ya kupeleka Wakenya hao ng’ambo.

Katika ripoti ya uchunguzi, Bunge la Kaunti ya Uasin Gishu lilipendekeza kuwa shirika hilo lipokonywe leseni na lishinikizwe kufidia zaidi ya vijana 200 waliodai kutapeliwa baada ya kuahidiwa kazi za maandalizi ya Kombe la Dunia nchini Qatar na ajira katika mataifa ya Ulaya.

Uchunguzi huo ulianzishwa baada ya vijana waliodai kutapeliwa na shirika hilo mwaka jana kuvamia afisi ya kamishna wa Kaunti ya Uasin Gishu wakitaka serikali iwasaidie kurejesha hela zao. Lakini shirika hilo limeshikilia kuwa madai dhidi yake ni porojo tu zinazosambazwa na washindani wanaolenga kuliharibia sifa.

Jambo la kushangaza ni kwamba asasi husika za serikali ya kitaifa zimesalia kimya na kuacha Bunge la Kaunti kuhangaikia madai.

Inawezekana kwamba madai yanayotolewa dhidi ya shirika hilo si ya kweli, lakini kuna haja ya serikali kubaini ukweli kwa kufanya uchunguzi wa kina.

Kumekuwa na malalamishi tele dhidi ya mashirika ambayo yamekuwa yakisafirisha Wakenya ughaibuni kusaka ajira.

Malalamishi hayo ya wakazi wa Uasin Gishu yanafaa kuwa kichocheo kwa serikali kumulika na kutathmini upya mashirika yanayopeleka Wakenya ughaibuni kusaka ajira.

Serikali, kupitia wizara ya Mashauri ya Kigeni, haina budi kuzingatia mapendekezo ya Kamati ya Bunge kuhusu Wakenya Wanaoishi na Kufanya Kazi Ughaibuni, iliyotaka leseni za mashirika yote ya kupeleka Wakenya nje kutafuta ajira, zifutiliwe mbali. Kamati hiyo inayoongozwa na Bi Haika Mizighi (Mwakilishi wa Kike wa Taita Taveta) ilishauri serikali kusajiri upya mashirika yanayosaidia Wakenya kupata kazi ng’ambo kama hatua mojawapo ya kupambana walaghai.

Mashirika kadhaa yamekuwa yakishutumiwa kwa kutelekeza Wakenya baada ya kuwafikisha ng’ambo na kuwaacha kuteseka mikononi mwa waajiri wao.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Dkt Alfred Mutua aliporejea kutoka Saudia Arabia mnamo Septemba 2022, alikiri kuwa ufisadi umekita mizizi katika sekta ya usafirishaji wa wafanyakazi ng’ambo.

Dkt Mutua alisema serikali ina kibarua kigumu kupambana na watu wenye ushawishi serikalini ambao wamekuwa wakisafirisha Wakenya ughaibuni kusaka kazi bila kuzingatia sheria. Waziri huyo sasa alainishe sekta hiyo jinsi alivyoahidi.

  • Tags

You can share this post!

Serikali ichunguze ‘shule bandia’ zinazodaiwa...

Surprise! Kidosho asakamwa kooni na pete ya uchumba

T L