TAHARIRI: Serikali ifanye juhudi kuzima mauaji ya watu

TAHARIRI: Serikali ifanye juhudi kuzima mauaji ya watu

Na MHARIRI

RIPOTI zinazotoka Lamu zinaonyesha kuwa hata kama serikali imeongeza maafisa wa usalama, bado maisha ya wakazi yanaendelea kuathiriwa.

Familia zaidi ya 300 zimetafuta hifadhi katiuka shule baada ya kutoroka nyumba zao.

Familia hizo, nyingi zikionekana za watu wanaoweza kuwa wanalengwa na wenyeji, zinaishi kwa hofu ya kuvamiwa zilikotorokea.

Katika eneo hilo la Lamu Magharibi, wengi waliokuwa wakitegemea shughuli kama uchimbaji mawe ya ujenzi kwenye timbo kati ya nyingine zizotekelezwa vichakani, sasa wameamua kutoenda kazini.

Mshirikishi wa eneo la Pwani, John Elungata alipozuru Lamu, alielezwa na kamishna wa kaunti kwamba huenda mauaji hayo hayatekelezwi na Al-Shabaab.

Kutokana na magaidi kushambulia Lamu mara kwa mara, inawezekana kuna watu wanaoendeleza ajenda za kisiasa kutumia jina la Al-Shabaab.

Kwanza inafahamika kuwa Al-Shabaab au magaidi wowote hufanya mambo yao kwa usiri mkubwa.

Huwa wanajitangaza tu baada ya kutimiza malengo yao.

Lakini katika mashambulizi ya Lamu, inasemekana watu hujitambulisha kuwa Al-Shabaab kabla ya kuwaua wanaowalenga.

Hapa ni wazi kuwa kuna ujanja fulani unaofanywa na watu wenye nia fiche.

Kama ambavyo baadhi ya wakuu wa usalama wanakisia kwamba huenda tatizo la umiliki wa ardhi linachangia, kuna haja ya upelekezi wa kina ili kufumbua fumbo hili.

Baadhi ya wenyeji wa Lamu wamekuwa wakilalamika kwamba, hata baada ya mahakama kuagiza walipwe fidia kwa kuipa serikali mashamba yao yatumiwe na mradi wa bandari ya Lamu (Lapsset), serikali haijawalipa.

Hata kama hali ni hiyo, kuwashambulia watu na kuwaua hakuwei kuwapa walalamishi fidia yao.

Jambo la kufanya ni kuwasilisha ujumbe maalumu kwa wahusika serikalini kupitia njia nzuri, ili suala la pesa zao lishughulikiwe.

Serikali ilipotangaza amri ya watu kutokuwa nje kati ya saa kumi na mbili alfajiri na kumi na mbili magharibi, ilitaka kuzuia mauaji hayo. Badala yake inasemekana watu wanashambuliwa mchana peupe.

Maafisa wa usalama walio katika kila pembe ya Lamu wanapaswa kushirikiana na wananchi na kuwa na urafiki nao, badala ua kuwaonyesha nguvu za vifaru na silaha.

Kuna haja ya kuimarisha doria na kukusanya habari za kujasusi kuhusu wahusika ambao huenda wanawafadhili wakazi kuendeleza uhasama wa kikabila.

Watakaogundulika kuhusika na uhuni huo, yafaa wakamatwe na kushtakiwa mahakamani ili wawe funzo kwa wengine.

You can share this post!

Majagina wapiga tizi kali tayari kuvaana na Uganda

Masomo yatatizika Lamu shule zikiwahifadhi waliokwepa...

T L