Makala

TAHARIRI: Serikali ifikirie tena juu ya ushuru mpya

August 8th, 2018 2 min read

Na MHARIRI

MPANGO wa serikali wa kujenga makazi mapya katika sehemu za miji nchini ni mzuri na bila shaka utakuwafaa mamilioni ya Wakenya wanaoishi katika mazingira ya kudhalilisha, hasa kwenye mitaa ya mabanda.

Ni wazi kwamb,a wengi wa wale wanaoishi katika vitongoji duni kama vile Kibera, Mathare na Mukuru Kwa Njenga wanafanya hivyo, sio kwa kupenda kwao bali kutokana na mapato yao madogo. Hivyo, hatua yoyote ambayo itawakweza kimaisha na kufanikisha ndoto yao ya kuishi kama binadamu wa kawaida inapasa kuungwa mkono kwa dhati.

Lakini kama ilivyo kawaida ya mipango yoyote yenye nia njema ambayo utekelezaji wake unazongwa na changamoto tele, mpango huu wa Serikali chini ya mwavuli wa Ajenda Nne Kuu za Serikali, huenda ukalemaa hata kabla ya kuanza kutekelezwa.

Kwanza, kuna uwezekano wa mahakama kuupiga breki kwa misingi ya ubaguzi wa wale watakaonufaika na makazi hayo mapya. Kwa sasa, wafanyikazi wote, katika sekta za umma na kibinafsi wanaolipwa mshahara wa Sh100,000 na zaidi, watalazimika kuchangia Sh500 kila mwezi huku mwajiri wao akiwasilisha kiasi sawa na hicho kwa hazina maalumu.

Lakini kinaya ni kwamba, watakaonufaika na mpango huo ni wale wanaopokea chini ya Sh99,000 kwa mwezi. Yaani, kimsingi ina maana kwamba, sehemu ya wafanyikazi watasaidia wenzao wenye mapato ya chini kupata makao mapya. Wazo zuri lakini lenye upendeleo mkubwa.

Kwa muda mrefu sasa, ujenzi wa makazi mapya umeachwa mikononi mwa watu na mashirika ya kibinafsi. Matokeo yake ni kwamba, wawekezaji katika sekta ya ujenzi wamelenga watu wenye mapato ya juu, na hivyo kupuuza sehemu kubwa na muhimu ya raia wa nchi wanaohitaji makazi safi na salama.

Kwa kweli waajiri katika sekta ya kibinafsi hawapaswi kutwikwa jukumu la kufadhili ujenzi wa makazi ambayo waajiri hao hawana mamlaka au ushawishi wowote kuamua kuhusu atakayenufaika na kwa wakati gani.

Isitoshe, ni kinaya kwamba serikali inaidai kimabavu mchango wa sekta ya kibinafsi katika ujenzi wa nyumba mpya ilhali haichangii chochote katika kuimarisha miundomsingi katika mitaa iliyojengwa tayari.

Mitaa mingi nchini, hasa inayokaliwa na wafanyikazi wenye mapato ya kadiri haina barabara na maji safi. Wakazi wengi wametumia raslimali zao kuchimba visima.

Kundi hili la wafanyikazi litanufaikaje na hazina hii ya ujenzi wa makazi? Hilo ndilo fumbo serikali inapasa kufafanua zaidi kabla kuendelea na mpango huu ambao malengo yake ni mazuri.