Makala

TAHARIRI: Serikali iige hisani yake Wanyama

August 1st, 2020 2 min read

Na MHARIRI

MIEZI michache baada ya kuahidi kujenga akademia ya michezo nchini, nahodha wa kikosi cha kitaifa cha soka, Victor Wanyama, ameanza kutekeleza ahadi yake.

Kapteni huyo wa Harambee Stars ambaye anasakata soka katika klabu ya Montreal Impact inayoshiriki Ligi Kuu ya Amerika (MLS), ameanza ujenzi wa akademia hiyo katika kaunti-ndogo ya Nambale, Busia, ikitarajiwa kuanza kuwasajili wanafunzi hapo Januari.

Hii ni hisani ya kupigiwa mfano hasa inapozingatiwa kuwa mzalendo mmoja anaweza kufanya jambo litakalochukua serikali nzima zaidi ya miaka 10 kutekeleza.

Mnamo 2013, serikali ya Jubilee iliahidi Wakenya kujenga akademia moja ya michezo na sanaa katika kila kaunti lakini hadi sasa – miaka saba baadaye – haijajenga hata taasisi moja ya aina hiyo.

Aidha serikali iliazimia kujenga angaa viwanja vitano vya hadhi ya kimataifa.

Kufikia sasa hakuna chochote kilichotimizwa mbali na kwamba hakuna dalili kuwa hata asilimia tano ya ahadi hizo itatimizwa.

Kwa mujibu wa mkandarasi, akademia hiyo inayojengwa katika ardhi ya ekari 20, itafungua milango yake kwa kusajili wanafunzi 50 kabla ya kuzidisha idadi hiyo kadri muda unavyosonga.

Kwa muda mrefu, tumekuwa tukisisitiza haja na umuhimu wa kuwapa watoto wenye talanta mbalimbali mazingira mwafaka ya kujiendeleza ili baadaye wafikie upeo wa vipaji vya. Lakini kwa bahati mbaya serikali imefumbia macho ukweli huo kwa kutoweka juhudi za kutambua na kukuza vipawa mapema.

Kwa bahati nzuri, Wanyama aliyewahi kuchezea Tottenham Hotspur na Southampton FC za Uingereza, ametuonyesha mfano. Sasa ni juu yetu kuiga mfano huo.

Yapo manufaa mengi zaidi kwa kutekeleza ahadi za serikali za kujenga akademia na viwanja.

Muhimu zaidi ni kuwa vipawa vitakavyonolewa katika taasisi hizo, vitaweza kupata ajira humu nchini na nje. Hii itasaidia kupunguza uhaba wa kazi hasa miongoni mwa vijana.

Pili ni kuwa taasisi hizo zenyewe zitawapa Wakenya wengi nafasi za kazi kama wakufunzi wa wanafunzi watakaojiunga nazo.

Juu ya yote, kwa kuanza kukuza kutambua na kukuza talanta kuanzia mashinani, hakuna shaka kuwa tutapiga hatua kubwa katika kabumbu ya kimataifa.