TAHARIRI: Serikali ijayo isuluhishe upesi mzozo na FIFA, klabu zinaumia

TAHARIRI: Serikali ijayo isuluhishe upesi mzozo na FIFA, klabu zinaumia

NA MHARIRI

HUKU Ligi Kuu ya Soka nchini ikitarajiwa kuanza kwa msimu mpya wa 2022/2023 Septemba 25, ni wazi kwamba athari za kupigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani FIFA zinazidi kukeketa klabu nyingi nchini.

FIFA ilichukua hatua hiyo mwaka 2021 baada ya kile ilichodai ni kuingiliwa kwa shughuli za soka na serikali, pale Rais wa Shirikisho la Soka Nchini Nick Mwendwa alipotimuliwa madarakani na hata kufunguliwa mashtaka ya ufisadi.

Lilikuwa jambo la kutamausha kuona mabingwa wapya wa Ligi, Tusker FC na Vihiga Queens wakikosa kutambisha soka ya haiba ya juu ya CAF licha ya kung’ang’ana kwa udi na uvumba kutwaa ubingwa.

Na sasa, klabu ya Wazito FC imetishia kususia kabisa kushiriki ligi hiyo wakilalamika kwamba marufuku yanayodumu kutoka FIFA yamezuia wawekezaji wa maana kujitokeza kufadhili klabu, hivyo basi kushindwa kuhimili mzigo mzito wa mishahara ya wachezaji na wafanyakazi wengine wa klabu.

Kila mdau na mfuatiliaji wa soka anafahamu ilivyo vigumu kutoa ushindani wa maana ligini bila ya kuwa na mdhamini anayeweza kusaidia kudumisha wachezaji wa haiba ya juu pamoja na kutumikia gharama nyinginezo ikiwemo kusafiri kwa mechi za mbali.

Wazito FC ndio wamejitokeza kueleza hofu hiyo na uwezekano wa kujiondoa kwenye mchuano wa ligi na labda klabu nyingine zinaweza pia kuchukua mkondo huo kutokana na ukweli uliopo wa uchechefu wa hela.

Ndio maana serikali inayokuja ambayo kufikia jana Ijumaa mshindi wa urais hakuwa ametambuliwa huku hesabu rasmi ya kura ikiendeshwa na IEBC, sharti huu mzozo baina ya serikali na FIFA utatuliwe haraka iwezekanavyo.

Waziri wa Michezo Amina Mohamed huenda alikuwa na nia nzuri ya kukabiliana na ubadhirifu wa fedha katika shirikisho hilo, lakini itabidi utawala mpya ujao uangalie jinsi utakavyorudisha FKF katika uhusiano mzuri na FIFA ili huduma za kawaida zirejeshwe.

Isisahaulike pia kwamba FIFA inaendesha miradi kadhaa haswa katika ukuzaji wa chipukizi kwa hivyo haipaswi kukaa muda mrefu huku suintofahamu hii ikizidi kushamiri.

Utawala mpya huenda ukalazimika kufanya mazungumzo mapya na shirikisho hilo la soka duniani na kuelewana kuhusu kuanzisha uhusiano upya kwa ajili ya kunusuru mustakabali wa soka, klabu na wachezaji ambao pia wanaumizwa na kukosekana kwa soka ya kimataifa kulikosababishwa na marufuku iliyopo.

La msingi ni kila mshikadau kuelewa hatari kubwa iliyopo endapo mzozo uliopo utaendelea bila kupata suluhu yoyote.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Uvutaji wa sigara maeneo ya umma...

WANDERI KAMAU: Wakenya wachukulie kwa uzito mchakato wa...

T L