TAHARIRI: Serikali ije na mikakati mipya kubabili utumizi wa mihadarati

TAHARIRI: Serikali ije na mikakati mipya kubabili utumizi wa mihadarati

NA MHARIRI

WIKI jana, walimu katka shule moja ya upili katika Kaunti ya Migori walimnasa mwanafunzi akiwa na misokoto ya bangi shuleni.

Awali, walimu katika shule moja ya upili Kaunti ya Vihiga walipata misokoto mitano ya bangi. Misokoto hiyo ilikuwa imeingizwa shuleni na wanafunzi walipotoka likizo fupi ya katikati ya muhula. Na mwezi Aprili wanafunzi wengine walikuwa wamenaswa wakiwa na bangi katika shule ya upili Kauntiya Kisii.

Visa hivi vya wanafunzi kuwa na bangi, vinathibitisha takwimu za Shirika la Kitaifa la Kukabili utumizi wa dawa za kulevya (NACADA), kwamba watumizi wakubwa wa mihadarati sasa hivi ni wanafunzi. Takwimu zilizotolewa mwezi Mei zinaonyesha kuwa wanafunzi walio na umri wa hadi miaka tisa, wanajihusisha na utumizi wa mihadarati, hasa uvutaji bangi, sigara na dawa za kusisimua hisia.

Kwa hivyo jana ulimwengu ulipoadhimisha Siku ya Kimataifa ya kupambana na Usafirishaji na Utumizi wa Dawa za Kulevya, macho yote hapa nchini yalipaswa kuelekezwa kwa vijana.

Tumekuwa na kauli kuwa vijana ndio viongozi wa kesho. Usemi huu una ukweli zaidi katika suala hili la utumizi wa dawa za kulevya.

Ripoti ya Afisi ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) inaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la watu wanaotumia mihadarati katika mataifa yenye pati la chini. Ripoti hiyo kwa jina “Global overview of drug demand and drug supply” inaeleza kuwa katika eneo la Afrika Mashariki, Kenya inaongoza kwa uvutaji bangi, utumizi wa kokeni na pia watu kujidunga sindano.

Data hii ya UNODC inafaa kutuzindua kama nchi. Wauzaji wa bangi na dawa nyingine za kulevya wanajua kuwa watu wanaoweza kuhadaiwa kwa urahisi ni wanafunzi.

Serikali siku za nyuma ilipiga marufuku uchuuzi wa vyakula na ikabomoa vioski karibu na shule. Hatua hiyo ililenga kuwakabili wauzaji dawa za kulevya kwenye sambusa, keki na vyakula vingine kwa wanafunzi.

Kama hatua hiyo imefanikiwa au la ni jambo linalohitaji kuangaliwa tena. Kilicho wazi ni kuwa, wahusika kwenye biashara ya mihadarati wamevumbua mbinu mpya za kuwapata wateja wao. Kama si hivyo, basi inakuwaje wanafunzi wanaorejea shuleni huwa na dawa hizi?

Shirika la NACADA, wizara za Elimu, Vijana na Afya zinapaswa kushirikiana na ile ya Usalama wa Ndani, kutafuta habari kuwahusu wahusika. Aidha, kampeni za baadhi ya wanasiasa kuhusu bangi na dawa za kulevya, yafaa zielezwe kwa njia inayoweka wazi kuwa japo ikiuzwa ng’ambo italeta pesa, bangi ni dawa ya kulevya iliyo na madhara kwa watumiaji.

You can share this post!

WANTO WARUI: Serikali ifanye ukaguzi wa kina wa majengo na...

WANDERI KAMAU: Wakati ni sasa kwa kina mama kujikweza na...

T L